Miaka mingi iliyopita, Mjusi na Chura walikuwa marafiki. Siku moja waliamua kuwatafuta wasichana wapenzi jijini.
Chura alimwonea Mjusi wivu. Mjusi alikuwa na ngozi iliyometameta na ya kuvutia.
Chura alimwuliza, "Ni kitu gani ulichofanya ukawa mrembo hivi? Hebu, nitazame, nina sura mbaya mno. Ninawezaje kuirembesha ngozi yangu?"
Mjusi alimjibu, "Sikiliza! Tia maji chunguni kisha ukiweke mekoni. Halafu u..."
Hakumaliza usemi wake. Chura alimjibu, "Ninajua tayari, najua. Fyata ulimi, rafiki yangu." Kisha aliondoka.
Chura alipofika nyumbani, aliyatia maji chunguni.
Maji yalipoanza kuchemka, alijitumbukiza ndani.
Ngozi yake ikachomeka na mkia wake ukakatika!
Na badala ya kumetameta na kuwa mrembo kama Mjusi, alikuwa na sura mbaya zaidi!