Hapo zamani, Kuku na Tai walikuwa marafiki. Siku moja, Tai alimkuta Kuku akiwa anapumzika chini ya mti.
Kuku alikuwa amesimamia mguu mmoja pekee.
Tai alimwuliza Kuku, "Mguu wako mwingine uko wapi?"
Kuku alimweleza Tai, "Mwenye duka aliukata na badala yake akanipatia vitu hivi."
Tai alimwuliza Kuku ikiwa yeye pia angeweza kufanya hivyo.
Tai vilevile alitaka mfuko uliojaa vitu. Kuku alikubali.
Tai alimwendea mwenye duka akitaka aukate mguu wake mmoja na badala yake ampatie vitu vitamu.
Mwenye duka alikubali akafanya hivyo.
Tai aliruka ruka kwa mguu mmoja akielekea nyumbani.
Hata hivyo, alivifurahia vitu alivopewa na mwenye duka.
Tai alipofika nyumbani, alimkuta Kuku akiwa na miguu yake miwili.
Tai alikasirika sana akaanza kumfukuza Kuku. Lakini hakuweza kumshika.
Hiyo ndiyo sababu Tai huwashambulia vifaranga wa Kuku kila mara. Anapomshika mmoja, yeye humla.