Kwa nini buibui ana miguu myembamba
Ghanaian folktale
Wiehan de Jager

Kulikuwa na buibui mmoja mvivu aliyeitwa Anansi.

Badala ya kujipikia chakula, Anansi alipenda kuwatembelea marafiki zake na kula chakula chao.

1

Siku moja, Anansi alipitia nyumbani kwa Sungura na kunusa mboga zilizokuwa zikipikwa. Alizitamani sana.

Sungura alimwambia, "Hazijaiva, lakini unaweza kunisaidia kuosha vyombo tukisubiri ziive."

Anansi akamjibu kwa haraka, "Samahani, nina kazi nyingine, nitarudi baadaye."

2

"Nitakujulishaje zitakapokuwa tayari?" Sungura akamwuliza.

Anansi akawaza kidogo halafu akasema, "Nitasokota utando nifunge ncha moja mguuni kwangu na nyingine chunguni. Mboga zitakapoiva, utauvuta utando, nami nitakimbia nije."

Kwa hivyo, Anansi aliufunga utando kwenye chungu kisha akaenda.

3

Anansi alimwona Kima na mkewe wakipika maharage. Kima alisema, "Jiunge nasi! Maharagwe karibu yaive."

Anansi akamjibu, "Samahani, nina kazi nyingine, nitarudi baadaye. Nitafunga ncha moja ya utando huu kwenye mguu na nyingine kwenye chungu chako. Maharagwe yatakapoiva, utauvuta utando, nami nitakuja."

4

Anansi alipita kwa Nguruwe na kunusia viazi vitamu. Nguruwe alisema, "Ninapika viazi vitamu na asali. Njoo tule."

Anansi akamjibu, "Ningependa lakini sina muda." Anansi akafunga utando ncha moja mguuni na nyingine kwenye chungu cha viazi vitamu.

Akamwambia Nguruwe, "Viazi vitakapoiva, utauvuta utando huu, nami nitakuja."

5

Anansi alipofika mtoni, miguu yake yote ilikuwa imefungwa kwa ncha za utando. Anansi akawaza, "Hili lilikuwa ni wazo zuri sana. Ila najiuliza ni chungu kipi kitakachoiva kwanza?"

Pale pale Anansi akahisi mguu mmoja ukivutwa. Akasema, "Aa, hii ni ncha ya utando uliofungwa kwenye chungu cha mboga."

6

Anansi aliendelea kuhisi mvuto baada ya mwingine. Alivutwa pande tatu mara moja. "Aa! Jamani!" Anansi alisema alipovutwa kwa mara ya nne.

Kabla hajapumua, akahisi ncha ya tano, ya sita, ya saba, na ya nane zikivutwa.

Anansi alivutwa huku na kule. Kila mmoja alivuta ncha yake wakati ule ule. Miguu yake ilivutwa ikawa myembamba.

7

Anansi alijirusha mtoni kwa haraka. Tando zote zilipochukuliwa na maji, alijivuta taratibu kwa maumivu hadi kando ya mto. Alihisi uchungu, "Aa! Aa!" Labda hili halikuwa wazo zuri kabisa."

Siku ile hakupata chakula chochote.

Tangu wakati huo, buibui huwa na miguu minane myembamba.

8
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Kwa nini buibui ana miguu myembamba
Author - Ghanaian folktale
Translation - Brigid Simiyu
Illustration - Wiehan de Jager
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs