Fisi, Sungura na beseni
Charles Katiwa Kiema
Salim Kasamba

Hapo zamani, Fisi na Sungura walikuwa marafiki sana.

Wote walikuwa maskini lakini Sungura alikuwa na punda. Pia alikuwa na beseni ndogo aliyoitumia kumlisha punda wake.

1

Adhuhuri moja, Sungura alitaka kumpatia punda wake maji. Hakuweza kutega maji kutoka kisimani kwa kutumia ile beseni yake ndogo.

Alienda kumwomba Fisi beseni yake kubwa. Fisi alimpatia kwa sababu ya urafiki wao.

2

Sungura alipomaliza kumnywesha punda maji, alikwenda nyumbani kwake na beseni ya Fisi.

Wiki mbili baadaye, Fisi alihitaji kufua nguo zake lakini alikumbuka kwamba Sungura alikuwa bado na beseni yake.

Fisi aliziacha nguo akaenda kwa Sungura kuichukua beseni yake.

3

Sungura alimrudishia Fisi beseni yake kubwa. Vilevile alimpa ndogo akisema, "Beseni yako ilizaa mtoto. Kwa sababu ya urafiki wetu, nimeamua kukupatia zote mbili."

Fisi alifurahi mno akazikubali beseni hizo mbili.

4

Siku mbili baadaye, Sungura tena alihitaji kumpa punda wake maji. Kwa mara nyingine, alimwendea Fisi amsaidie.

Fisi aliwaza, "Kwa sababu nitapokea beseni moja zaidi, nitampa tena beseni yangu!"

Sungura aliichukua beseni kubwa ya Fisi kumnyweshea punda wake maji. Baadaye, aliipeleka nyumbani kwake.

5

Fisi alisubiri kabla kwenda kuichukua beseni yake kwa Sungura. Alitaka izae nyingine kama mbeleni!

Fisi alipoenda nyumbani kwa Sungura kuichukua beseni yake, Sungura alisema, "Fisi, rafiki yangu, nilikuwa ninajitayarisha kukuletea ujumbe mbaya. Beseni yako ilikufa siku mbili zilizopita. Si unajua kwamba vitu vyote vilivyo hai lazima vife?"

6

Fisi hakuweza kuamini aliyoyasikia. Alisema, "Lazima niwaite wanyama wakubwa waje kuamua kesi hii."

Fisi aliwaita tembo, viboko, vifaru na twiga. Walifika nyumbani kwa Sungura kuamua kesi.

7

Sungura aliulizwa kueleza kilichotokea. Alisema, "Mara ya kwanza nilipoomba beseni ya Fisi, ilizaa mtoto nami nilimpatia zote mbili. Nilipoomba mara ya pili, beseni hiyo ilifariki kabla kuzaa. Kwa sababu chochote kilicho hai, vilevile hufa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa!"

Wanyama wote walikubaliana na Sungura. Fisi aliipoteza beseni yake.

8
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Fisi, Sungura na beseni
Author - Charles Katiwa Kiema
Illustration - Salim Kasamba
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs