Adun, mrembo
Taiwo Ẹhinẹni
Wiehan de Jager

Adun alikuwa msichana mrembo sana.

Wanaume kutoka kijijini kwao, walipenda wamuoe.

Lakini, Adun aliwakataa wote.

1

Mamboleo aliomba miguu kutoka kwa mwanamume mmoja, mikono kutoka kwa mwingine, na kiwiliwili kutoka kwa mtu tofauti.

Siku ya soko, aliziunganisha sehemu hizo. Akakiweka kichwa chake juu yake halafu akaenda sokoni.

2

Mamboleo alimtaka Adun na alikuwa na azma ya kumuoa. Adun alipendezwa na Mamboleo akataka kuolewa naye.

Ingawa Mamboleo alitoka mji wa mbali, Adun alikuwa tayari kurudi naye kwake.

3

Adun na Mamboleo walipokuwa wakisafiri, mwenye miguu aliichukua.

Kisha mwenye mikono akaichukua mikono yake.

Mwishowe kabisa, mwenye kiwiliwili alikichukua.

4

Kichwa pekee kilibaki kikaendelea kutembea na Adun.

Ingawa Adun aliogopa, hakutoroka.

Baadaye, waliwasili nyumbani kwa kichwa hicho.

5

Keshoye kabla ya kichwa kuondoka kwenda shambani, kilimweleza Kobe, "Adun akijaribu kutoroka, ipulize pembe hii unijulishe."

6

Kichwa kilipoondoka, Adun alifunganya virago vyake akitaka kutoroka.

7

Kobe alipoona hivyo, aliipuliza pembe akisema, "Kichwa, kichwa, Adun yu karibu kutoroka."

8

Kichwa kilimwendea Adun na kusema, "Unadhani unaenda wapi?"

Adun alirejea nyumbani kwa kichwa, shingo upande.

9

Hatimaye, Adun alitafuta mawaidha kutoka kwa mganga.

Mganga alimshauri, "Nenda ununue keki za maharagwe. Ziloe katika mafuta kisha uziweke ndani ya ile pembe anayoipuliza."

10

Adun alifuata maagizo ya mganga.

Aliziweka keki zilizoloa mafuta ndani ya ile pembe.

11

Asubuhi ilipofika, Adun alivichukua virago vyake akaanza kutoroka tena.

Kobe aliichukua pembe tayari kuipuliza. Lakini, keki tamu zilianguka mdomoni kwake kila alipoipuliza.

12

Kobe alizila na kuzila zile keki.

Adun alitoroka akaenda zake.

13
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Adun, mrembo
Author - Taiwo Ẹhinẹni
Translation - Ursula Nafula
Illustration - Wiehan de Jager
Language - Kiswahili
Level - First paragraphs