Nelima atajirika
Salaama Wanale
Mango Tree

Hapo zamani za kale, kulikuwa na yatima wawili, Nelima na Nambuye. Waliishi katika shamba lisilokuwa na rutuba.

Kwa muda mrefu nchi ilishuhudia ukame nao hawakuwa na chakula. Walilazimika kwenda mbali kutafuta chakula.

1

Nelima alikuwa mnyamavu, mnyenyekevu na alipenda kusaidia.

Nambuye, dadake, alikuwa mwenye kiburi na hakumsikiza yeyote. Hakuwajali watu wengine.

2

Siku moja, Nelima na Nambuye walipoamka, walitambua kwamba hawakuwa na chochote cha kula.

Walilazimika kutafuta chakula. Kila mmoja alikwenda kutafuta upande tofauti.

3

Wakati huo huo, aliishi Bi Kizee mmoja aliyeitwa Netasile. Netasile alikuwa na ugonjwa wa ukoma na mwili wake ulijaa vidonda.

Watu wa kijiji chake walikuwa na imani kuwa Netasile angeweza kumpa mtu utajiri.

4

Alipokwenda kutafuta chakula, Nambuye alikutana na Bi Kizee Netasile.

Netasile akamwita, "U hali gani mwanangu? Unatoka wapi na unakwenda wapi?"

5

Nambuye alijibu maswali yote kwa dharau.

Netasile hakusita, akasema, "Nibebe unipeleke nyumbani kwangu nami nitakwambia la kufanya."

6

Nambuye akasema kwa kiburi, "Heri nife kuliko kuvigusa hivyo vidonda vyako."

Bi Kizee alipuuza maneno hayo akamtakia safari njema.

7

Nambuye aliendelea kutembea. Alifika mahali palipokuwa na majongoo, nyoka, mabuu na wadudu wengine.

Alikuwa amechoka na kudhoofika kwa kukosa chakula. Alipoketi chini kupumzika, wadudu walianza kumuuma.

8

Nelima naye alikutana na Netasile. Alifurahi kwani Netasile alikuwa binadamu wa kwanza aliyekutana naye tangu aanze safari yake.

Netasile akamwita na kumwuliza, "U hali gani mwanangu? Unatoka wapi na unakwenda wapi?"

9

Nelima alijibu kwa upole. Netasile akasema, "Nipeleke nyumbani nami nitakwambia la kufanya."

Nelima alimpeleka. Netasile akasema, "Umenitendea lile wengi wemeshindwa kufanya."

Alimpa Nelima kijiti ambacho kingemsaidia kupata vyote alivyotaka.

10

Nelima alimshukuru Bi Kizee na kuelekea nyumbani.

Alipofika nyumbani, alipata nyumba mpya iliyojaa vitu aina aina na chakula kingi.

Tangu siku hiyo, Nelima akawa tajiri.

11

Nelima hakufurahia kumpoteza dadake lakini alisema, "Asiyesikia ushauri huishia ndani ya kinywa cha ndovu."

12
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Nelima atajirika
Author - Salaama Wanale
Translation - Brigid Simiyu
Illustration - Mango Tree
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs