

Hapo zamani, familia moja ilikuwa na mti wa matunda matamu yaliyowavutia wengi kutaka kuyaonja.
Familia hiyo pia ilikuwa na binti mzuri mrembo. Urembo wake na tabia zake nzuri vilisifiwa na watu wengi.
Alipokua mtu mzima, wanaume, vijana kwa wazee, walienda kwao wakiwa na nia ya kumposa.
Wazazi wa yule msichana walifanya uamuzi. Mwanamume ambaye angeketi pale nyumbani siku nzima bila kula tunda lolote, angeozwa binti wao.
Habari hiyo ilisambaa kijiji kizima. Mtu wa kwanza kufika alikuwa kiongozi wa wakulima wote kijijini.
Alikuwa tajiri mwenye sura nzuri tena alikuwa angali kijana. Alikaribishwa akaandaliwa matunda.
Lakini, kabla ya muda kupita, aliyala matunda kisha akaagwa akaenda zake.
Aliyefuata alikuwa kiongozi wa wafugaji. Yeye pia alikuwa tajiri mwenye sura nzuri na alikuwa angali kijana.
Msichana alipendezwa naye. Lakini alipoandaliwa matunda, aliyala mara moja.
Yeye pia aliagwa akaenda zake.
Wa tatu alikuwa na mashamba mengi, lakini, jeuri na mwenye sura mbaya. Msichana aliomba Mungu yule mtu ale matunda upesi ili aweze kwenda zake.
Alipoandaliwa matunda, alikataa kula. Wakati ulipopita, msichana alimwomba ale. Ilipofika saa kumi, alizidiwa na njaa akala.
Yeye pia aliagwa akaenda zake.
Aliyefuata, alikuwa mzee mwenye sura mbaya, mlaji rushwa asiyekuwa na adabu. Hakupendwa na yeyote kijijini. Msichana alitumaini angekula moja kwa moja na kwenda zake.
Alipoandaliwa matunda alikataa kula. Ilipofika saa kumi na mbili ya jioni, aliomba kwenda haja. Aliporudi, alinukia matunda huku midomo yake ikiwa na rangi nyekundu!
Msichana alifarijika mzee alipoagwa na kwenda zake.
Siku chache zilipita kisha mwana wa mfalme, aliyekuwa kijana, tajiri na mwenye sura ya kupendeza, alifika.
Msichana alimtazama akapendezwa naye mno. Msichana alimpeleka faraghani akamwomba asile matunda. Alimwandalia matunda machache kuliko waliyoandaliwa waliomtangulia.
Ilipofika adhuhuri, alikuwa amekwisha kula akaagwa. Msichana masikini alilia machozi ya hasira na hasara.
Siku iliyofuata, mkulima masikini na mvivu alifika pale. Alikuwa mwenye sifa ya kubobea maneno ambayo yaliwafurahisha watu. Akafika akiwa na nia madhubuti kushinda.
Msichana naye alimwandalia matunda mengi akamwomba ale aende zake. Alikataa kula. Msichana alisubiri kwa hofu.
Saa sita alikuwa hajala. Ilipofika saa kumi, aliomba maji.
Msichana alimwomba Mungu ale, lakini hilo halikutendeka.
Wazazi wa yule msichana hawakuwa na budi ila kumkubali "yule mvivu." Msichana naye alitamani kunusurika na mtu yule, lakini wazazi hawakuweza kumsaidia.
Walipokuwa njiani kwenda kwao nyumbani, mkulima alipiga makofi akiimba wimbo mzuri ambao uliwavutia watu waliokuwa barabarani.
Miongoni mwa watu wale walikuwa watumishi wa mwana mfalme. Walimwita mkulima wakamhonga kwa pesa pamoja na ng'ombe mradi akubali kumwacha msichana.
Bila kusita, akakubali pesa pamoja na ng'ombe akaenda zake peke yake.
Watumishi wale walimvisha msichana libasi murua mno wakampeleka mpaka jumba kubwa la mfalme.
Muda si mrefu, wazazi wake waliitwa na harusi ikaandaliwa.
Niliwaacha wakisherehekea nami nikaja kuwahadithieni ninyi.

