

Hapo zamani katika kijiji cha Lunyiko, kuliishi mwanamme aliyeitwa Ndong'a.
Ndong'a na mkewe Namukaywa walikuwa na binti sita.
Namukaywa alipokuwa na mimba ya saba, Ndong'a alimwonya, "Ukimzaa msichana tena, nitakuua. Lakini ukinipa mtoto mvulana, nitakuandalia karamu kubwa!"
Wakati wa kujifungua ulipowadia, Namukaywa alienda kwa mkunga wa kienyeji.
Je, mtoto atakuwa msichana au mvulana?
Walikuwa mapacha! Mvulana alimwita Mukhwana, na msichana akamwita Mulongo.
Alimtazama Mukhwana kwa furaha. Alipomtazama Mulongo, alihuzunika mno.
Ni jambo moja tu angelifanya.
Namukaywa alimwacha Mulongo chini ya ulezi wa mkunga.
Akampeleka Mukhwana nyumbani kwa mumewe.
Kwa fahari, alimwonyesha Ndong'a mtoto mvulana.
Alifurahi sana na kuwaita wanakijiji kusherehekea kuzaliwa kwa mtoto wake mvulana.
Mukhwana alikua na kuwa kijana mwanamume wa kupendeza.
Na Mulongo naye, akawa mwanamke mrembo mno.
Siku moja wakati alikuwa akichunga mifugo wa babake, Mukhwana alimwona msichana mrembo sana.
"Huyu ndiye msichana ningependa kuoa," alijiambia.
Lakini alipomwuliza kumuoa, aliimba hivi:
Mukhwana wetu, Mukhwana
Mama alionywa na baba
Akijifungua mvulana
Ampeleke nyumbani
Akiwa msichana, atauawa.
Hii ilifanyika tena na tena. Mukhwana hakujua la kufanya.
Alimwendea mamake, Namukaywa, akasema, "Nimempata msichana mrembo ambaye ningependa kumuoa. Lakini kila ninapomwuliza, anaimba wimbo ule ule."
La kushangaza, Namukaywa alisema, "Anachoimba msichana yule ni kweli. Yeye ni dadako. Mlizaliwa mapacha. Babako alimtaka mtoto mvulana na wala si msichana. Nilimwacha dadako kwa mkunga nikakuleta wewe nyumbani."
Wakati Mukhwana alimwambia babake kisa hicho, babake aliona kwamba alikuwa amefanya kosa.
Alimwita Namukaywa, na pamoja walienda kwa mkunga kumleta Mulongo.
Mulongo alipofika nyumbani, babake na wazee wa kijiji walimchinja mbuzi.
Walitekeleza kimila cha kumwunganisha Mulongo na ndugu zake saba.
Mwaka mmoja baadaye, Mulongo aliolewa kwa mwana wa tajiri kutoka kijijini.
Aliiletea familia yake furaha na mali mengi.
Wote waliishi maisha ya furaha.

