Mti ulionusuru kijiji cha Balantu
Karen von Wiese
Julia te Water Naude

"Shhhu!" Bibi alisema. "Kuna joto kali. Na chungu hiki ni kizito sana. Hebu tupumzike kidogo chini ya kivuli cha mti." Alijipangusa jasho usoni huku akiegemea mizizi ya mti.

Sela naye alisimama huku ameushika huo mbuyu kwa mkono mmoja. Nduguye, Tovo, aliuzungukazunguka ule mbuyu akiangalia ukubwa wake.

"Bibi, mbuyu huu ni mzee sana, sivyo?" "Ndiyo, Sela. Lakini sio mzee au mkubwa zaidi ya mbuyu ulio katika kijiji cha Balantu!" "Balantu? Kijiji hicho ki karibu?" Sela aliuliza. "Tafadhali tueleze kuhusu mti huo," Tovo alisema.

"Basi ketini msikilize," Bibi alisema huku akianza kuwahadithia.

1

Katika kijiji cha Balantu kuliishi msichana aliyeitwa Hami. Siku moja, Hami na ndugu yake Angula, walienda kuchota maji.

Hami alipokuwa akijaza chungu chake, Angula alimwona sungura. Alimkimbiza, lakini hakuweza kumshika.

Sungura alikuwa na mbio kumshinda.

2

Chungu cha Hami kilijaa maji. Sasa alikuwa tayari kwenda nyumbani. Aliangalia kila upande akamkosa Angula. Hakujua alikokwenda. Aljiua kwamba hangeenda nyumbani bila nduguye mdogo.

Alitazama kila mahali lakini hakumwona. Alipomtafuta, alimpata akiwa amelala kwenye nyasi nyuma ya kichuguu kikubwa.

Alipokuwa anamkaribia, Angula alimwashiria kwamba anyamaze. Mbona anyamaze?

3

Karibu na pale kulikuwa na kundi la vijana. Walikuwa wamebeba mishale, nyuta na mikuki! Hami aliweza kusikia sauti zao.

"Angula," Hami alimwita kwa sauti ya chini. "Wanaume hao ni wezi wa mifugo. Wamekuja kuiba ng'ombe wetu na kuchoma nyumba zetu. Njoo haraka. Lazima tukimbie nyumbani tukawatahadharishe wanakijiji."

Basi waliondoka polepole kutoka eneo hilo kisha wakakimbia kwenda nyumbani.

4

Hami alimwita mjomba kwa sauti, "Mjomba, kimbia, kimbia! Kuna wanaume wamekuja kuiba ng'ombe na kuteketeza nyumba." Mjomba alimrudisha ng'ombe kijijini.

Hami alimwita shangazi, "Shangazi, kimbia, kimbia!" Wanume wanakuja kuiba ng'ombe wetu na kuteketeza nyumba zetu!" Shangazi alichukua jembe lake, akambeba mtoto aliyekuwa akilala kisha akurudi kijijini.

Hami akamwona babu yake akiwa na punda wake. Akamwita kwa sauti, "Babu, kimbia, kimbia, wanaume wanakuja kuiba ng'ombe wetu na kuteketeza nyumba zetu."

Babu alimpiga punda akaenda mbio kuelekea kijijini.

5

Hami na nduguye wakafika kijijini. Hami akawaita watu wote kwa sauti, "Kimbieni, kimbieni. Kuna wanaume wanaokuja kuiba ng'ombe wetu na kuteketeza nyumba zetu!"

Wanakijiji wakawa na hofu sana. Wakawa wamechanganyikiwa kama kundi la mchwa lililokanyagwa na ng'ombe. Hawakujua pa kujificha wala la kufanya.

Wangewaficha ng'ombe wao wapi? Wangezificha nafaka zao wapi?

Wangejificha wapi wao wenyewe?

Hami aliogopa sana.

6

Akakumbuka mahali ambapo yeye na Angula walikuwa wakienda kucheza wakati mwingine.

Mahali salama.

Mahali pa siri.

7

"Ninapajua mahali ambapo sote tunaweza kujificha!" Lakini wanakijiji hawakumsikiliza. Walikuwa wakipiga kelele sana.

Sasa angefanyaje ili wamsikilize? Unadhani Hami alifanya nini?

Alichukua ngoma na kuipiga kwa nguvu kabisa. Bam! Bam! Bam! Boom! Boom! Boom!

Wanakijiji wote walitulia. Hami akawaambia kwa sauti, "Ninajua mahali ambako tunaweza kujificha. Nifuateni."

8

Hami alimshika Angula mkono akasema, "Njoo tawapeleke wanakijiji kwenye mti wetu. Sote tutakuwa salama huko."

Angula alitikisa kichwa. "Hapana, Hami. Mahali hapo ni siri yetu. Ulisema tusimwambie mtu yeyote."

"Ndiyo", Hami akasema. "Ilikuwa siri yetu. Lakini sasa sote tuko hatarini."

9

Hami na Angula waliwaongoza wanakijiji. "Kwa nini unatuleta hapa? Hatuwezi kujificha hapa," walisema.

Hami akamwita babake, "Nitakuonyesha." Hami na babake waliingia wakashuka ndani kupitia shimo dogo. Pale chini kulikuwa na uwazi mkubwa. "Lakini watu wote hawawezi kuingilia kwenye shimo dogo pale juu," babake alisema.

"Hapana," Hami alisema. "Tutaleta shoka tutengenze mlango wa kuingilia hapa kwenye shina."

Walitengeneza kiingilio shinani. Wanakijiji wakaleta vyakula na vyombo vya kupikia. Wote wakaingia ndani ya uwazi mkubwa wa mbuyu. La kushangaza ni kwamba kulikuwa na nafasi ya kuwatosha wote.

10

Wakati jua lilipotua na giza kutanda, kijiji kizima kilitulia tuli! Ulikuwa usiku wenye baridi.

Wale wahalifu walitembea taratibu kuelekea kijijini.
"Lazima wanakijiji wawe wamelala sasa," waliambiana.

Nao wanakijiji walijificha ndani ya mti. Nini kingetokea? Walihisi baridi na woga.

Hami akasema, "Kuna baridi sana. Tuwashe moto." Akachukua mawe mawili akayachua, moja juu ya jingine haraka haraka.

11

Baada ya muda mfupi, cheche za moto zikashika nyasi.

Kisha moto mkubwa ukawaka wakaanza kuota.

12

Nje, wavamizi walizidi kukaribia. Ghafla, mmoja wao alipiga mayowe akionyesha mbuyu walimojificha. Ndimi za moto zilitoka mle. Macho makali yaliangaza kutoka mle. Moshi ulipaa angani.

"Ni jinamizi kubwa!" Walilia kwa woga. Kwanza mvamizi mmoja aligeuka na kukimbia. Kisha mwengine, na mwengine. Hadi wote wakaenda zao.

Watu wa kijiji cha Balantu wakaokolewa.

13

Bibi akanyamaza. Wakati huu wote Sela alikuwa anashikilia shina la mbuyu.

"Kwa hivyo, ni mti huo uliowaokoa wanakijiji." Bibi akamaliza kuwahadithia.

14
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Mti ulionusuru kijiji cha Balantu
Author - Karen von Wiese, Beryl Salt, Muhdni Grimwood, Barbara Meyerowitz
Translation - Mutugi Kamundi
Illustration - Julia te Water Naude
Language - Kiswahili
Level - Read aloud