Paka na Mbwa ni marafiki
Yamkela Mbhele
Busisiwe Ndlovu

Paka na Mbwa ni marafiki wazuri.

Waliamua kumtembelea rafiki yao, Kuku, siku ya kuzaliwa kwake.

Kuku aliishi katika kijiji kingine. Paka na Mbwa wangesaifiri kwa siku mbili ili kufika huko.

1

Paka na Mbwa walikuwa na tabia tofauti sana.

Mbwa alipenda kula na kulala na mara nyingine alikuwa mkorofi kidogo.

Paka alikuwa mwema, mkarimu na wa kutegemewa.

Walikutana nyumbani kwa Mbwa kupanga safari yao.

2

"Nitaleta chakula cha siku ya kwanza," Mbwa alijitolea.

"Nitaleta cha siku ya pili," alisema Paka.

Wakaandika kila kitu ili wasisahau.

3

"Itakuwa ya kusisimua kumuona Kuku hivi karibuni. Imekuwa muda tangu tumuone rafiki yetu," Mbwa alisema alipokuwa akimsindikiza Paka nyumbani.

"Asante kwa kunisindikiza nyumbani," Paka alimwambia Mbwa.

4

Walikutana mapema sana siku iliyofuata kuanza safari yao.

Waliimba na kucheza kwa furaha njiani.

Baada ya muda, walipumzika chini ya mti mkubwa. "Nina njaa! Tule," Paka alisema.

5

Mbwa aliharakisha kuweka chakula kwenye bakuli mbili. Chakula kilikuwa cha mafuta mengi na chenye maji maji.

Paka akauliza, "Hiki ndicho chakula ulichotuletea sisi wawili?"

Paka alikasirika kwa sababu rafiki yake hakuleta chakula walichokubaliana. Hakula chakula cha Mbwa.

6

"Kwa nini unasubiri?" Mbwa aliuliza. Alitumaini kwamba Paka angeacha kulalamika na kula, badala yake.

Kwa hasira, Paka akauliza, "Kwa nini ulileta chakula unachopenda wewe tu?"

Mbwa alikuwa anakula kwa haraka sana hadi bakuli likateleza.

Chakula chote cha Mbwa kilimwagika chini.

7

"Usijali rafiki yangu," Paka alisema.

Paka alitoa sandwichi nzuri sana. Akaanza kula.

Mbwa alitazama chakula cha Paka kwa tamaa.

Paka alipomaliza kula, alipakia vitu vyake na akamwambia Mbwa, "Tunaweza kuendelea na safari yetu?"

8

Hawakuzungumza kwa kipindi chote kilichosalia cha safari. Tumbo la Mbwa lilinguruma kwa njaa.

Jioni hiyo, Paka alijipakulia chakula mwenyewe. Alilala kwa furaha kwa sababu alikuwa ameleta chakula cha kutosha.

Mbwa alilala njaa.

9

Asubuhi, Paka alijipakulia kifungua kinywa kidogo. Mbwa hakuacha kutazama chakula cha Paka.

Paka alimpatia Mbwa chakula.

Mbwa alisema, "Nisamehe. Nilikuwa na ubinafsi sana."

Paka alijibu, "Tule pamoja."

Waliketi chini kula.

10

Walipoendelea na safari yao, walikuwa marafiki tena!

Walifika nyumbani kwa Kuku kwa wakati.

"Safari yenu ilikuwa aje rafiki zangu?" Kuku aliuliza.

Wakitabasamu, Paka na Mbwa walijibu, "Nzuri sana."

11

Kwa hakika ilikuwa sherehe nzuri ya siku ya kuzaliwa.

Walikula, wakaimba na wakacheza!

12
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Paka na Mbwa ni marafiki
Author - Yamkela Mbhele
Translation - Anne Kamau
Illustration - Busisiwe Ndlovu
Language - Kiswahili
Level - First paragraphs