Tunaishi kwenye Manyata
Nina Orange
Arthur Makali

Watu wanaishi katika aina nyingi tofauti za nyumba. Baadhi ya watu wanaishi katika nyumba zilizojengwa kudumu kwa muda mrefu. Wengine wanaishi katika nyumba ambazo hazidumu kwa muda mrefu.

Kitabu hiki kinahusu makazi ya muda yanayoitwa manyata, ambayo yanaundwa na vibanda vya kitamaduni.

1

Manyata hii ipo kaskazini ya kati ya Kenya, katika Kaunti ya Samburu. Kuna vibanda kumi kwa jumla. Dada Sidai na Naeku wanashiriki kibanda kimoja, na wazazi wao na kaka yao mdogo wanashiriki kibanda kingine.

Mjomba wao na kaka zao watatu wakubwa wanakaa kwenye vibanda vingine, pamoja na familia zao

2

Familia hizi hulisha ng'ombe wao pamoja na kusaidiana. Hawakai sehemu moja kwa muda mrefu. Wanahama ili kutafuta maeneo mapya ya malisho kwa ajili ya ng'ombe.

Kuzunguka manyatta kuna uzio wa matawi ya miiba. Uzio huu unasaidia kuwazuia ng'ombe wasitoke nje na kuwazuia wageni wasiingie ndani

3

"Tunaanza mchakato wa ujenzi kwa kukusanya vifaa kutoka kwenye mazingira yetu. Tunakusanya matawi ya miti ili kujenga muundo wa msingi wa kibanda," anasema Sidai.

Naeku anaongeza, "Tunajua jinsi ya kutumia vifaa vya asili kujenga nyumba zetu. Kila mtu katika manyatta anasaidia katika ujenzi.

4

Tunatumia matawi makubwa kutengeneza fremu imara ya kuta. Tunafunga fremu ya paa kwenye fremu ya kuta kwa kutumia mizizi, na hivyo kutengeneza fremu thabiti kwa kibanda chote," anaelezea Sidai.

"Vibanda vina paa za chini, na hivyo ni vigumu kwa upepo kuvipindua," anaongeza Naeku.

5

Sidai anaendelea, "Mara fremu ya kibanda inapokuwa imesimama, tunashona matawi membamba kati ya matawi makubwa."

Naeku anaongeza, "Tunatengeneza tabaka nene za nyasi na kuzifunga kwenye fremu ya paa. Hii inaitwa kuezeka."

"Kuezeka vizuri kunatulinda kutokana na mvua na jua," anaongeza Sidai.

6

Sidai anaongeza, "Paa za vibanda vyetu zinaweza kuwa tambarare au mviringo."

Naeku anasema, "Kupaka tope ni sehemu ninayopenda zaidi ya ujenzi. Tunachanganya matope na samadi kutengeneza plasta ya asili. Tunapaka plasta hii kwenye fremu ya kuta, tukijaza nafasi zilizopo. Hii husaidia kuzuia upepo na mchanga kuingia ndani."

7

Sidai anaendelea, "Kupaka plasta kwenye kuta kunaziba kuta hizo mara tu zinapokauka. Pia tunapaka plasta juu ya uso wa kuta. Plasta iliyokauka ni ngumu na imara."

Naeku anaongeza, "Hakuna madirisha kwenye kuta, lakini kibanda chetu kina mlango wa mbao."

8

"Upakaji wa plasta kwenye kuta husaidia kuzuia-joto kibandani," anasema Sidai. "Neno 'kuzuia-joto' linamaanisha nini?" anauliza Naeku.

"Kuta za matope na samadi husaidia kuweka kibanda kuwa baridi ndani wakati nje ni joto. Katika hali ya hewa ya baridi, kuta zinasaidia kutuweka joto ndani kwa kuhifadhi joto la moto," anajibu dada yake.

9

"Watu wote katika manyata wanashiriki katika ujenzi, na sote tunasaidia kuvunja vibanda tunapohama.

"Sio vigumu kuvunja miundo na kutumia sehemu hizo tena mahali pengine," Sidai anaeleza.

10

"Vifaa vyetu vya ujenzi ni vyepesi, kwa hivyo ni rahisi kuvibeba. Tunatumia ngamia au punda kubeba vifaa vyote muhimu kutoka manyata yetu ya zamani. Kwa mfano, paa lenye nyasi," anasema Sidai.

"Pia tunaweza kukusanya vifaa vingi zaidi vya ujenzi kutoka kwenye mazingira mapya," anaongeza Naeku.

11

"Nyumba yetu inatufaa tunavyoishi, ambayo ni kuhama hama na mifugo yetu," anasema Sidai.

"Kuhama hama kunamaanisha hatuwezi kwenda shule na marafiki zetu daima," anasema Naeku.

"Shule yetu inaturuhusu kuomba vitabu, na tunajaribu kufuatilia masomo yetu," anamalizia Sidai.

12
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Tunaishi kwenye Manyata
Author - Nina Orange, Ursula Nafula
Translation - Anne Kamau
Illustration - Arthur Makali
Language - English
Level - Longer paragraphs