

Siku ya Haki za Kibinadamu huadhimishwa nchini Afrika Kusini kama sikukuu ya umma tarehe 21 Machi kila mwaka.
Kitabu hiki cha hadithi kinahusu historia na umuhimu wa Siku ya Haki za Kibinadamu.
Katika enzi za ubaguzi wa rangi, Waafrika weusi wa Afrika Kusini walikandamizwa.
Watu wengi walipigana dhidi ya ubaguzi wa rangi. Walikuwa wakipigania haki na usawa.
Siku ya Haki za Kibinadamu, tunakumbuka wale waliopigania uhuru.
Mnamo Machi 21 mwaka wa 1960, watu huko Sharpeville na Langa walikwenda kwenye maandamano.
Walikuwa wakipinga sheria za ubaguzi wa rangi, zisizo za haki, hasa 'sheria ya pasi'.
Waandamanaji walipiga kelele wakisema, "Nguvu! Zetu! Nguvu kwa watu!"
Huko Sharpeville, watu walikuwa wakiimba na kuandamana kwa amani hadi kituo cha polisi.
Polisi waliwashambulia waandamanaji.
Baadhi ya waandamanaji walijeruhiwa na wengine wakapoteza maisha yao.
Machi 21 ilikumbukwa kama Siku ya Sharpeville.
Baada ya 1994, ilifanywa kuwa likizo ya umma kama Siku ya Haki za Kibinadamu.
Ilikuwa ni njia ya kusema asante kwa watu waliopigania uhuru.
Watu walioandika Katiba mpya ya Afrika Kusini walitaka kila mtu aheshimu haki za kibinadamu.
Katiba ya kidemokrasia inatuambia haki na wajibu wa watu wote. Kila mtu ana haki sawa.
Kila mwaka, Machi 21 ni likizo ya umma. Ofisi na shule huwa zimefungwa.
Ni siku ya kusherehekea haki za kibinadamu. Ni siku ya kusherehekea usawa.
Watu husherehekea na kuheshimu siku hii kwa njia tofauti.
Watoto wanaweza kusherehekea siku hii muhimu kwa kuzungumza juu ya haki zao.
Ndiyo, watoto pia wana haki!
Haki za watoto ni aina maalum ya haki za kibinadamu, kwa watu chini ya miaka 18.
Watoto wote wana haki. Je, unazijua haki zako?
"Haki ya kutunzwa," anasema Ntombi.
"Haki ya kuwa na jina!" anapiga kelele Sikuku
"Haki ya kuishi katika nchi yangu, au nchi yoyote," anasema Shadrack.
"Haki ya kupata elimu," anasema Arnold.
"Haki ya kuwa salama," Melanie anasema, kutoka nyuma.
"Haki ya KUTOjeruhiwa au kunyanyaswa," anasema Nalayiselo.
Hizo ni baadhi ya haki ambazo watoto wanazo. Sisi sote tuna haki na pia tuna wajibu.
Je, watoto wana majukumu gani?
"Wajibu wa kufanya kazi zangu za nyumbani," Ann asema.
"Jukumu la kuwatendea wengine tunavyotaka watutendee," anasema Cheyeza.
"Jukumu la kujitunza na kuwa na afya njema," anasema Sikuku.
"Wajibu wa kufanya vyema shuleni niwezavyo," anasema Miso.
"Wajibu wa kuheshimu haki za wengine," anasema Lerato.
Siku ya Haki za Kibinadamu inatukumbusha kuwa sheria inawapa watu wote haki sawa. Daima tuheshimu na kulinda haki za kibinadamu.
1. Kwa nini tarehe 21 Machi ni sikukuu nchini Afrika Kusini?
2. Haki za kibinadamu ni nini?
3. Toa mifano mitatu ya haki za watoto.
4. Tafuta ujumbe kuhusu Mswada wa Haki za Afrika Kusini. Tengeneza orodha ya haki.
Vitabu katika mfululizo huu
Siku ya Upatanisho
Siku ya Uhuru
Siku ya Urithi
Siku ya Haki za Kibinadamu
Siku ya Wanawake
Siku ya Wafanyakazi
Siku ya Vijana
Hadithi hii ilitayarishwa na kuandikwa kwa lugha ya Xitsonga kama sehemu ya mradi wa nyenzo za kusoma za Zenex Ulwazi Lwethu mnamo 2020.

