Biashara ya Akoro ya ndizi
Mele Joab
Atilabachew Reda

Akoro ni mumewe Chichi. Wanaishi katika kijiji kiitwacho Kanam katika Kaunti ya Turkana.

Akoro ana bustani ya ndizi inayompatia mazao mazuri.

1

Siku moja kabla jua kuwa kali, Akoro aliondoka akibeba kreti ya ndizi mbivu kichwani kwake.

Alitembea kwa ujasiri akielekea sokoni Kilindo, umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwake.

2

Wanaume na wanawake wa umri wake walimtazama kwa mshangao. Baadhi yao hata walimcheka kwa sauti, "Bila shaka Akoro amerogwa. Anawezaje kufanya kazi kama hii? Wanaume kutoka jamii yetu hawauzi ndizi!"

Lakini, Akoro hakujali. Alikuwa ameamua kuifanya kazi yoyote kwa bidii.

3

Alipowasili sokoni tu, Akoro alizipanga ndizi zake kisha akaketi karibu nazo akisubiri wateja.

Alijiuliza, "Kuna yeyote atakayezinunua ndizi zangu?"

4

Dakika chache baadaye, mwanamke aliyevalia rinda la kizambarau, alikikaribia kibanda cha Akoro. "Unauza ndizi kilo moja pesa ngapi?" mwanamke yule aliuliza.

"Shilingi hamsini, dadangu," Akoro alimjibu kwa heshima.

5

Mwanamke yule akasema, "Tafadhali nifungie kilo moja na nusu. Lakini, lazima unipunguzie bei."

Akoro akamjibu, "Hakuna shida dadangu, nitapunguza shilingi kumi. Wewe ni mteja wangu wa kwanza." Akoro alimpatia mwanamke yule ndizi zake.

6

Akoro alianza kufurahia biashara yake. Wanunuzi walivutiwa na ndizi zilizopendeza na maneno ya Akoro matamu.

7

Adhuhuri, Akoro alikuwa amechoka kusimama. Alikikalia kigoda akaendelea kuuza ndizi zake. Mwanamke aliyevalia rinda la bluu, alinunua ndizi nyingi.

Waliomcheka Akoro, walianza kushangaa jinsi biashara yake ya ndizi ilivyonawiri.

8

Saa tisa alasiri, Akoro alimuuzia mwanamke aliyekuwa akitoka kazi ndizi zake za mwisho.

Aliwapa ndizi mbili mbili wanaume walioketi naye wakati huo wote. Walimtumbuiza kwa hadithi tamu alipowasubiri wateja.

9

Akoro alliondoka na kreti tupu kichwani. Alitembea akiimba wimbo wa furaha akijivunia kazi aliyoifanya siku hiyo.

Aliwaza, "Kufanya bidii kwa dhati ni jambo muhimu maishani."

10

Aliinunulia familiia yake unga wa mahindi, mafuta ya mboga, chai, sukari na mkate.

Kisha alienda nyumbani kwa furaha. Mawazo yake yalijaa mipango ya kuipanua biashara yake ya ndizi.

11
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Biashara ya Akoro ya ndizi
Author - Mele Joab
Translation - Ursula Nafula
Illustration - Atilabachew Reda, Natalie Propa
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs