

Hapo kale kuliishi mtu maskini na mkewe. Walikuwa na mtoto mmoja aliyeitwa Nonkungu.
Nonkungu alikuwa mrembo na mkarimu. Wazazi wake walimpenda sana.
Siku moja, wazazi wa Nonkungu waliamua aende kuishi kwa mjombake tajiri aliyeitwa Mtonyama.
Mama alimshonea Nonkungu rinda akalirembesha kwa shanga. Pia, alimtengenezea mkufu wa shanga.
Nonkungu alisafiri hadi akaufikia mto. Akavuka kwa kukanyaga mawe.
Alipofika upande ule mwingine wa mto, alikutana na msichana aliyekuwa amevaa matambara.
"Unaenda wapi?" yule msichana mdogo alimwuliza.
"Ninaenda kuishi kwa mjombangu Mtonyama," Nonkungu alisema.
"Ala! Mtonyama ni mjombangu pia. Nami ninaenda kumtembelea," yule msichana akajibu.
Baada ya kutembea pamoja kwa muda, yule msichana akasema, "Rinda lako ni zuri na mkufu wako pia unapendeza. Hebu nivae nione jinsi mavazi hayo yatakavyonifaa."
Nonkungu akavua mkufu wake na rinda lake akampa yule msichana mdogo.
Msichana huyo alipovua matambara yake na kuvaa nguo za Nonkungu, Nonkungu aligundua kwamba huyo msichana alikuwa na mkia!
Sasa alifahamu kuwa yule hakuwa msichana bali alikuwa jitu.
Walipotembea kwa muda, Nonkungu alimwambia, "Tafadhali, nirudishie mkufu na rinda langu."
Imbulu alijibu, "Acha niendelee kuvaa hadi tuufikie ule mti."
Walipofika kwenye mti, Nonkungu alimwambia Imbulu, "Tafadhali, nirudishie rinda na mkufu wangu."
"Acha nivae hadi pale kwenye ule mto."
Nonkungu alikubali kwa woga.
Hatimaye, waliufikia mto. Kwa mara nyingine, Nonkungu alimwambia imbulu, "Tafadhali, nirudishie mkufu na rinda langu."
Hata hivyo Imbulu alimjibu, "Niruhusu nivae hadi tuufikie ule mji."
Walipoufikia mji, Imbulu alimsukuma Nonkungu nyuma akawaambia wanawake waliokuwa nje, "Mtazameni msichana huyu aliyevaa matambara. Amekuwa akinifuata siku nzima. Nataka aniondokee."
Nonkungu aliaibika akakimbia na kujificha.
Imbulu alimwambia Mtonyama, "Mimi ndiye mpwa wako, Nonkungu. Ulivyopanga na wazazi, wamenituma nije niishi hapa kwako."
Familia ya Mtonyama ilimkaribisha bila kujua ni imbulu.
Maskini Nonkungu alilala nje akila chakula cha mbwa.
Wakati wa mchana Nonkungu alitembea huku akiimba:
Matatizo, matatizo!
Wazazi walinituma,
Kwa mjomba Mtonyama,
Kakutana na imbulu,
Nguo zangu kachukua,
Matatizo, matatizo!
Siku moja, nduguye Mtonyama alikuwa akipita. Akasikia wimbo mtamu ukiimbwa. Hakujua mwimbaji.
Alirudi akamweleza Mtonyama kuhusu wimbo aliousikia. Mtonyama naye alikwenda akausikiliza wimbo kwa makini. Akamwona Nonkungu.
Nonkungu alimweleza kwamba Imbulu alichukua nguo zake maridadi akambadilishia na matambara.
Mtonyama alimchukua akampeleka nyumbani akamficha. Mtonyama alijua jinsi angefanya kumwadhibu imbulu.
Mtonyama alikuwa amesikia kwamba mkia wa imbulu ulipenda maziwa sana. Hangeyapita maziwa bila mkia kunywa kidogo.
Aliwaambia wafanyakazi wake wachimbe shimo refu na kulijaza na maziwa lala. Kisha aliwaita wasichana wote wa kijijini kwa mashindano ya kuliruka lile shimo.
Imbulu aliogopa. Hakutaka kuliruka lile shimo. Alijua mkia wake ungetamani maziwa lala. Alijificha, akaufunga mkia wake, akiukazia kwenye mwili wake kabisa.
Baadaye alijiunga na wasichana wengine kuliruka shimo.
Wasichana waliliiruka shimo mmoja baada ya mwingine.
Ilipokuwa zamu ya Imbulu, alijaribu kuruka juu ya shimo lakini mkia wake ulifunguka ukamvuta chini, chini, chini kwenye shimo la maziwa lala.
Imbulu alipokuwa akitapatapa ndani ya maziwa lala, waliliziba lile shimo kwa udongo. Na huo ndio uliokuwa mwisho wa imbulu.
Naye Nonkungu aliishi na mjombake Mtonyama kwa furaha na starehe kwa miaka mingi.
Na huo ndio mwisho wa hadithi.

