

Ilikuwa harusi ya kwanza katika familia ya Tenana. Refi alikuwa amechangamka sana.
"Nitakuwa msaidizi wa Elsa nikiwa nimevaa nguo na viatu vipya!" Refi aliwaelezea kuku wake. Aliwaelezea kuku wake kila kitu.
Babake alikuwa amempa kuku kama zawadi alipokuwa akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake. Refi aliwapenda sana.
"Refi, waondoshe hapo hao kuku wachafu!" Mamake alipiga kelele, "Siwataki popote karibu na hema la harusi."
Refi aliwafukuza kuku kutoka kwenye hema. "Tokeni enyi viumbe washienzi," alisema. "Singependa mliwe wakati wa harusi ya Elsa."
"Mama asema kwamba hii itakuwa harusi ya kufana zaidi katika kijiji cha Mailisaba," Refi aliwaambia kuku wake. "Pia anasema kwamba ninaweza kuwasaidia wasichana wale wakubwa kupika." Kuku hawakumsikiliza hata kidogo.
"Refi!" Mamake alimwita kutoka ndani, "Tafadhali acha hao kuku. Njoo unichungie chungu!"
Mamake Refi alijivunia nyumba yake na alitaka iwe safi siku ya harusi. Alisafisha, akaosha na kusugua kila kilochokuwamo. Alipomaliza, hapakuwa na chembe cha vumbi popote.
Kuku walipochokoa vichwa mlangoni, Mamake Refi alipiga mayowe, "Tokeni nje ninyi viumbe vyenye miguu na midomo michafu!"
Refi aliwafuata kuku wake hadi kwenye jua. "Mama anasema ukweli, mnaaibisha," aliwakemea.
Refi alitabasamu kisha akaenda kujaza ndoo maji. Alikuwa na wakati mgumu kuwashika kuku wake. Hawakudhani kwamba ilikuwa jambo zuri wao kuoga.
Refi alimweka kuku wa kwanza ndani ya ndoo ya maji. "Kaa wima, ewe kiumbe shenzi," alipiga kelele. "Haitachukua muda mrefu kukuosha!"
Refi alipopangusa pua na macho ya kuku, ghafla kuku alikuwa dhaifu akaanguka kando ya ndoo. "Huu sio wakati wa kulala," Refi alisema.
Alimtikisa kuku kwa nguvu ili maji yote yadondoke. Kisha akamlaza juu ya nyasi ili akauke. Kuku alitulia pale akiwa amelala.
Aliwaosha kuku wote wanane na kuwaweka mstari mmoja juu ya nyasi ili wakauke. Hakuna yeyote aliyepapatua hata unyoya mmoja.
"Nitawaacha mlale kwa muda mfupi," Refi aliwaza. Alienda kukitazama chungu kilichokuwa mekoni.
Shangazi zake Refi, yaani Mama Netty na Mama Teddy, walikuwa wakitayarisha harusi ya Elsa.
Walitakiwa kufanya matayarisho hayo kwa pamoja lakini hawakupendana hata kidogo.
Mama Netty aliwaona kuku wa Refi wakiwa wanakauka. "Hiki ni chakula kizuri kwangu. Nitawapeleka nyumbani!" Alijiambia.
Alilichukua kanga lake na kuwafungia kuku wote mle ndani. Hakuna kuku hata mmoja aliyesonga. "Sawa kabisa!" Alitabasamu. "Sasa nitawaweka mahali ambapo Mamake Teddy hatawahi kuwapata."
Alikiweka kifurushi hicho pembeni kati ya maboga."
Mama Teddy aliamua kutayarisha kitoweo alichokipenda. Alikwenda katika bustani ya maboga. Alikiona kifurushi cha Mama Netty chini ya mboga.
Alipokifungua, kuku wote wanane walianguka nje. "Esh!" Alipiga kelele huku akiruka nyuma kwa mshangao. "Ah, ninyi ndio kuku wasafi kuliko wote! Mko tayari kwa chungu changu," aliwabembeleza. "Sasa nitawaficha wapi wapenzi wangu?" Mama Teddy alicheka. "Lazima nipate mahali pazuri kabisa," alisema huku akitembea nyumbani.
"Ninajua," alisema hatimaye, "Nitawaweka paani!" Mama Teddy alipanda juu akawaweka kuku katika mstari kwenye paa la nyumba ya nyasi.
Siku iliyofuata, jua lilichomoza kwa wakati mzuri kwa harusi. Refi alikuwa wa kwanza kuamka na kwenda kuwatazama kuku wake.
Hakuwapata mahali alikuwa amewaweka. "Lazima wawe wamekauka vizuri kwa sasa. Nina hakika wameenda kutafuta kifungua kinywa chao," alisema.
Harusi ya Elsa ilikuwa ya kufana. Wale kuku hawakuamka kutoka paani. Kwa hivyo, hawakujiunga na wasichana wasaidizi wa bi-harusi walipoingia wakicheza.
Hakuna kuku yeyote aliyetikisika wakati kwaya ya kanisa iliimba kwa sauti ya juu nyimbo nzuri za kuvutia. Walikuwa bado wanalala juu ya paa wakati Padre alihubiri.
Hawakutikisa hata unyoya wakati nguruwe na babu yake Refi walipokoroma mahubiri yalipoendelea.
Hakuna hata mguu mmoja wa kuku uliotetemeka wakati kondoo waliranda na kuingia ndani ya hema wakiwa karibu kuangusha keki ya harusi.
Wakati babake bwana harusi alipokuwa katikati ya hotuba yake ndipo mambo yalianza kubadilika paani.
Kuku wa kwanza aliyanyoosha mabawa yake na kuruka kwenye kifua cha Mamake Molly.
Mama Teddy aliyekuwa amekaa karibu naye alianza kucheka. Kuku mwingine alirukia kitambaa kipya cha Mama Netty. Watu waliokuwa kwenye meza nyingine walizuia kicheko.
Mwanamke aliyekaa karibu na Mama Netty aliweka kichwa chake chini ya meza, "Ai, aai, aaaaii, he, he, heeeeeeee!" Alicheka.
Wale kuku wote waliamua kujiunga na wale wawili wa kwanza.
Hungeweza kumwona Mama Netty kwa sababu alikuwa amefunikwa na kuku hao wote!
Wageni walicheka kwa mayowe. Wanaume walilazimika kuzishika tumbo zao. Wanawake waliviringika katika viti vyao.
Vijana walijishikilia kwa wenzao. Akina nyanya hawangeweza kupumua kwa ajili ya kucheka. Akina babu walitikisa fimbo zao.
Halafu, shangazi hao wawili walitazamana wakaanza kucheka pia.
Mama Teddy aliufungua mdomo wake wazi kwa kicheko.
Mama Netty alikirusha kichwa chake nyuma na kucheka hadi mashavu yakatikisika.
Refi hakuamini!
Wageni wote walikubaliana kwamba hiyo ilikuwa harusi nzuri zaidi iliyowahi kufanyika kijijini Mailisaba.
"Aa, mna bahati sana! Refi aliwaambia kuku wake alipokuwa anawaweka kwenye chumba chao usiku ule.
"Mama anasema kuwa hatawahi kuwaweka kwenye chungu chake."
"Lakini, tazama jinsi mlivyo wachafu tena," aliwaambia.
"Nadhani nitalazimika kuwaosha tena kesho!"

