Mulongo na Fisi
Sarah Nangobi
Wiehan de Jager

Palikuwa na msichana aliyeitwa Mulongo.

Aliishi na wazazi wake karibu na kijiji cha Budongo.

Siku moja mamake Mulongo alimtuma kuchota maji kisimani.

1

Njiani, alikutana na marafiki zake wakienda msituni kutafuta kuni.

Mulongo alitaka kwenda nao. "Tafadhali, nisubirini hapa! Lazima nimchotee mama maji kwanza." Mulongo aliwasihi.

Lakini marafiki zake hawakutaka kusubiri.

2

"Sawa, nitawakuta huko msituni!" Mulongo alisema huku akikimbia kwenda kumchotea mamake maji.

Baadaye, alienda msituni kuwatafuta marafiki zake.

3

Alifuata njia iliyoelekea kwenye kijito. Upande mwingine wa kijito kulikuwa na njia nyingine ndogo kila mojawapo ikielekea upande tofauti.

"Njia ipi marafiki zangu walifuata?" Mulongo alishangaa.

4

Aliichagua njia iliyokuwa pana kisha akatembea, na kutembea, lakini hakuwapata marafiki zake.

Alichoka sana kwa hivyo alipopumzika chini ya mti.

Alilala muda mfupi baadaye.

5

Mulongo alipoamka, ilikuwa giza. Gizani, macho ya manjano yalimulika. Alikuwa amezungukwa na fisi!

Aliogopa asiweze hata kulia. Alijaribu kukimbia, lakini fisi walimzunguka wakionyesha wazi kuwa walikuwa na njaa.

6

"Usisonge," sauti ya fisi mkubwa zaidi ilisikika. "Ukikimbia, utaliwa!"

"Tafadhali, niache niende nyumbani!" Mulongo aliwasihi.

7

Badala yake fisi walimpeleka Mulongo katika nyumba yao iliyokuwa msituni. Chumba hicho kichafu kilijaa mifupa na kelele za nzi.

Mulongo alilala chini na kujifanya kuwa amepatwa usingizi.

8

Gizani, aliwasikia fisi wakiongea wenyewe kwa wenyewe. "Moto unaendelea vipi? Je, maji yanachemka?" Mmoja aliuliza."

Mwingine aliJibu, "Kila kitu ni tayari. Nimlete sasa?"

"Ndiyo, ndiyo! Tunahisi njaa!" Fisi wale wengine walinguruma.

9

Walikuwa karibu kumvuta Mulongo kumtoa chumbani wakati fisi mkubwa aliongea, "Fisi, subirini. Kumbuka kanuni ya kijiji. Hakuna fisi anayekubaliwa kula peke yake. Ni lazima tuialike jamii nzima kushiriki mlo."

10

Waliokwenda kuwaalika jamii, hawakurudi haraka. Yule fisi mkubwa alianza kusinzia na kukoroma pale mbele ya moto.

Hii ilikuwa nafasi nzuri ya Mulongo kutoroka! Lakini angempitaje yule fisi?

Umbo lake kubwa lilifunika sehemu yote ya mlango.

11

Njia ilikuwa ni moja tu. Alijihimiza na kurukia juu ya mgongo wa fisi kwa mara moja.

Kisha, akakimbia, na kukimbia jinsi miguu yake ilivyomwezesha.

12

Wakati huo huo, fisi wale wengine walirudi na kuona kilichotokea.

Walimfuata huku wakipiga kelele za hasira na gadhabu.

Lakini, walikuwa wamechelewa.

13

Alipokaribia kijiji chake, wanakijiji walimtambua na kushangilia wakisema, "Mulongo, Mulongo anakuja, Mulongo anakuja."

Wazazi wake walikimbia kumbusu huku wakishukuru Mungu kwa kumwokoa mototo wao, "Mulongo, tulidhani umekufa!"

14

Kutoka siku hiyo, Mulongo na watoto wengine hawakuwahi kururdi msituni peke yao.

15
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Mulongo na Fisi
Author - Sarah Nangobi
Translation - Brigid Simiyu
Illustration - Wiehan de Jager
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs