

Siku moja, Buibui Anansi, alivuna viazi vikuu shambani mwake.
Vilipendeza na kuonekana vitamu sana.
Alivichoma taratibu kwenye moto na akaanza kula.
Buibui Anansi alipokuwa akitia tonge la kwanza kinywani, mlango wake ulibishwa. "Lo! Lo! Lo!" alisema moyoni. "Huyo ni nani?"
Kasa, aliyeonekana mchovu, alisimama mlangoni. Kasa alisema, "Anansi, tafadhali niruhusu niingie. Nimetembea mwendo mrefu leo. Nimechoka na ninahisi njaa."
Buibui Anansi alimruhusu Kasa akaingia.
Buibui Anansi hakumgawia mwengine chakula chake kitamu, hata mgeni.
Kasa alipotaka kula, Buibui Anansi alimkemea, "Kasa, huwezi kula kwa mikono michafu. Nenda ukanawe kwanza."
Mikono ya Kasa kweli ilikuwa michafu sana kwani aliitembelea siku nzima. Kasa alijikokota hadi mtoni akanawa mikono kisha akarudi.
Buibui Anansi alibaki akibugia viazi kwa haraka. Kasa aliporejea hakupata kiazi hata kimoja.
Kasa alimwambia Buibui Anansi, "Asante kunialika kwa chakula cha jioni. Nami pia nitakukaribisha kwangu nikuandalie chakula kitamu."
Kasa alijikokota kuelekea nyumbani kwake.
Siku moja Buibui Anansi aliwasili nyumbani kwa Kasa kabla chakula cha jioni. Kasa alikuwa amejilaza chali akiota jua kama Kasa wafanyavyo.
Alipomwona Buibui Anansi, alisema, "Aa! Hujambo Anansi! Umekuja kushiriki nami chakula cha jioni?"
Buibui Anansi akaitikia, "Naam, nitafurahia sana, asante."
Anansi alikuwa akihisi njaa mno.
Kasa alipiga mbizi na kuzama chini ya mto akaandaa chakula cha jioni. Naye Buibui Anansi alingoja kando ya mto.
Baada ya maandalizi, Kasa alirudi juu ya maji akasema, "Kila kitu ki tayari, karibu. Twende tukafurahie mapochopocho."
Kasa alipiga mbizi tena na akaanza kula majani matamu aliyokuwa ameandaa.
Buibui Anansi alijaribu kujizamisha mtoni lakini, wapi! Yeye alikuwa buibui wala sio kasa. Alishindwa kupiga mbizi kabisa. Kila alipojaribu, alielea juu ya maji.
Alijaribu kuruka majini tena na tena lakini ng'o! Hakufanikiwa kukifikia chakula kilichoandaliwa na Kasa chini ya maji.
Hatimaye, Buibui Anansi alipata wazo zuri. Alitia mawe kwenye mifuko ya koti lake. Akawa mzito akaweza kuzama majini. Alikuwa mwerevu kwelikweli!
Sasa aliweza kuiona meza iliyojaa majani matamu na laini pamoja na vyakula vingine vya kupendeza. Alidondokwa na mate alipoviona vyakula hivyo.
Buibui Anansi alipokuwa akinyoosha mkono kuchukua chakula hicho cha kupendeza, Kasa alimkataza akisema, "Anansi, unawezaje kula ukiwa umevaa koti? Haiwezekani hapa kwangu."
Bila kufikiri, Buibui Anansi akasema, "Samahani! Bila shaka usemavyo ni kweli. Sikufikiria kuhusu hilo." Buibui Anansi, alilivua koti lake.
Punde tu alipolivua koti, Buibui Anansi alielea juu ya maji kwa sababu hakuwa na mawe ya kumwezesha kuzama.
Alihuzunika na akachopeka kichwa chake majini akawa anamtazama Kasa akila chakula hicho chote kitamu peke yake.

