

Hapo zamani za kale, mtu na mkewe walikuwa na watoto wa kiume saba wajinga.
Watoto hao waliipoteza mifugo, walivunja jembe, na kila mtu aliwadanganya walipokuwa sokoni.
Mama yao aliomba, "Ee Mungu, mbona watoto wangu wote ni wajinga? Tafadhali, nipe angaa mtoto mmoja mwenye hekima."
Mwanamke huyo alijifungua mtoto mvulana. Mtoto huyo alikuwa mdogo mno.
"Tutamwita Kadogo," mama akasema.
Kadogo hakukua kimo bali aliongezeka umri. Alikuwa mwerevu sana. Wazazi wake walimpenda lakini, nduguze walimwonea wivu.
"Mbona wazazi wetu wanakupenda wewe zaidi yetu sisi?" Walimwuliza Kadogo. "Hebu jitazame! Wewe ni mdogo kama panya."
Kulikuwa na adui aliyeishi karibu na familia ya Kadogo. Siku moja, nduguze Kadogo waliwaza, "Adui yetu ana ng'ombe wengi wanono. Usiku wa leo twendeni tukawaibe fahali wawili. Tutamtumia punda wa baba kubeba nyama zote."
Hawakumwona Kadogo kwa sababu alikuwa nyuma ya kigoda cha baba yao.
Usiku huo, nduguze Kadogo walimchukua punda wakaenda kwa adui yao.
Kadogo aliwafuata mbio ila hawakumwona.
Walipofika kwa adui, lango lilikuwa limefungwa. Ndugu hao hawakuweza kuingia ndani. Mmoja wao akasema, "Heri tusingemuacha Kadogo nyumbani. Yeye ni mwerevu na angeweza kuingia ndani."
Hawakuwa wamemwona Kadogo kwa sababu alikuwa amejificha.
Kadogo alijitambulisha, "Ndugu zangu, sikubaki nyumbani. Nisubirini hapa nami nitaingia ndani niufungue mlango. Nitawaelekeza fahali wote kwenu."
Ndugu wa tatu aliuliza, "Utaingiaje ilhali lango limefungwa?"
Kadogo alicheka akasema, "Tazama, kuna mlango unaonitosha mimi."
Nduguze walipotazama, waliona nafasi ndogo karibu na lango. Ni nafasi iliyotosha paka pekee, lakini Kadogo aliweza kupita.
Kadogo alipenya kwenye nafais hiyo. Alipanda juu ya lango na kulifungua.
Aliwaongoza fahali kutoka nje bila tatizo. Alisema, "Nendeni, fahali wangu wazuri! Nendeni nje!"
Mmoja wa nduguze adui alikuwa amelala katika chumba chake. Mbwa waliokuwa macho walianza kubweka walipomsikia Kadogo.
Bwana wao aliamka na kuuliza, "Kunaendelea nini hapa?"
Kadogo alipomwona, alijifanya kuwa mmoja wa wafanyakazi. "Usiwe na wasiwasi, bwana mkubwa. Fahali wetu wawili walikuwa wamepotea. Sasa ninawarejesha," alisema.
Bwana yule alikasirika akasema, "Wacha kupiga kelele. Tunataka kulala." Alirudi chumbani kwake, akaufunga mlango.
Kadogo aliwaongoza wale fahali wawili nje. Nduguze walifurahi sana. "Tazama fahali hawa ni wanono! Hebu tuwachinje tule nyama sasa," walisema.
Kadogo alijibu, "Adui wetu akituskika atatoka nje tena. Lazima tuvuke mto tuwapeleke mbali."
Kadogo na nduguze waliwapeleka fahali mbali na nyumba ya adui. Walipofika kwenye mto, wale ndugu saba walitazama maji kisha wakatikisa vichwa vyao.
"Hatuwezi kuuvuka mto huu. Maji haya ni mengi na hatujui kuogelea. Kadogo yuko wapi? Yeye ndiye atakayejua jinsi ya kuvuka ng'ambo."
Kadogo alikuwa ameketi juu ya pembe za fahali.
Alisema, "Niko hapa, ndugu zangu. Ninajua la kufanya. Nipeni ukambaa." Ndugu zake walimpatia ukambaa.
Kadogo aliufunga ukambaa upande mmoja wa mti. Kisha akwaambia nduguze, "Ushikeni ukambaa huu mvuke mto. Mtakuwa salama."
Mmoja baada ya mwingine, ndugu wale waliushika ukambaa wakavuka mto. Fahali waliogelea mbele yao.
"Sasa tuko mbali na adui wetu. Tunaweza kuwachinja fahali," Kadogo alisema. Wale ndugu waliwachinja fahali wakazigawa nyama mafungu saba kila mmoja na lake.
Kadogo aliwauliza, "Li wapi fungu langu?"
Nduguze walicheka wakasema, "Fungu lako? Wewe ni mdogo sana. Huwezi kula nyama hii. Kadogo, wewe huna nyama."
Kadogo alikasirika mno akawaza, "Nitawaadhibu kwa kunitendea hivi." Aliwaambia, "Ikiwa hamtanipa nyama, nipeni kibofu cha fahali mmoja."
Ndugu hao walimtupia Kadogo kibofu na wakaondoka. Kadogo alikichukua kile kibofu, akakimbia mbele ya nduguze. Alipanda mti uliokuwa karibu na njia waliyopitia.
Kadogo aliufunga upande mmoja wa kibofu kisha akakipuliza hadi kikawa kama mpira. Akakichukua kijiti akaanza kukipiga kile kibofu.
Alipokuwa akikipiga kile kibofu, Kadogo alisema, "Tafadhali bwana, sikuwaiba fahali wako. Ni ndugu zangu waliowaiba. Wamewaua fahali wako na kuzigawanya nyama!"
Nduguze Kadogo walilia, "Adui wetu ametufuata. Atatuadhibu!" Kisha wakatoroka.
Kadogo alishuka kutoka mtini huku akitabasamu. "Nyama yote itakuwa yangu sasa," alisema.

