

Zamani za kale, kulikuwa na kijiji kimoja katika Kaunti ya Turkana.
Wanakijiji walikutana kila jioni kucheza ngoma ya kienyeji iitwayo edonga.
Wachezaji wa kijiji hicho walifahamika kila pahali.
Walikuwa na ustadi mkubwa wa kucheza ngoma ya edonga.
Watu kutoka vijiji jirani walifika kijijini humo kucheza ngoma hiyo.
Siku moja, mgeni aliyeusikia umaarufu wa ngoma hiyo ya edonga, alituma mjumbe wake aende kuipeleleza.
Mjumbe alipofika, wanakijiji walijawa na hofu. Wakajiuliza, "Huyo mgeni ni nani? Mbona amemtuma mjumbe wake?"
Wanakijiji walijitayarisha kama kawaida. Walimchinja mbuzi na kupika chakula kingi.
Vilevile walikutana wakaandaa kafara na kusubiri siku nzima hadi jioni ila mgeni hakufika.
Walicheza ngoma kama kawaida hadi usiku wa manane.
Usiku huo kulikuwa na wachezaji ngoma wengi na kila mtu alikuwa amesisimka.
Kabla ya ngoma kuisha, mgeni alifika.
Kwa mavazi alifanana na wanakijiji, kwa hivyo, hawakumtambua.
Alipopata nafasi ya kucheza ngoma, alijiunga na wanaume wengine.
Ilionekana wazi kuwa alicheza tofauti na wenyeji.
Watu waliaanza kumcheka. Wachezaji wengine walicheka wakiwa wamepiga magoti. Wengine walikaa kitako. Wengine walianguka chini.
Mgeni alikasirika alipochekwa. Akaamua kuwalaani.
Aliacha kucheza ngoma ghafla. Mara hiyo hiyo, kila mchezaji akabadilika kuwa jiwe.
Waliolala, waliosimama, waliokaa kitako na waliopiga magoti, wote walibaki walivyokuwa.
Kisha mgeni akatoweka kijijini.
Mawe hayo yamebaki mahali pale hadi wa leo.
Saa za usiku husikika yakiimba na kucheza edonga.
Hiyo ndiyo asili ya Namorutunga.

