

Hapo zamani za kale, Simba alikuwa mwenye nguvu aliyeogopwa kuliko wanyama wote. Angeweza kuwashika wanyama wengine na kuwala.
Asubuhi moja alipokuwa akitafuta kifungua kinywa, alinaswa katika mtego wa mwindaji.
Simba alipiga mayowe kwa uchungu. Alivuta ili kujinasua kutoka mtegoni. Mtego ulinasa mguu zaidi kila alipovuta.
Mwishowe, Simba alipokuwa amechoka na kuhisi uchungu, alikata tamaa.
Siku zilivyopita ndivyo Simba alichomwa kwa jua. Alihisi njaa na kiu na wala hakuwa na mwokozi.
Alipozidi kuwa mnyonge aliwaza, "Nitakufa kwa njaa na kiu."
Asubuhi moja, Simba alisikia sauti kichakani. Alisikiliza na kuchunguza kwa karibu.
Aliona Ngiri akitembea na mkwewe na watoto wakizungumza na kucheka.
Ngiri na familia yake walikuwa wanaenda mtoni kunywa maji na kucheza topeni kabla ya jua kuwa kali.
"Ngiri, tafadhali niokoe kutoka mtegoni." Simba alimsihi.
"Kamwe sitakuokoa! Wewe mnyama katili. Nikikuokoa utanila mimi na familia yangu kama kifungua kinywa."
"Naahidi kamwe sitatenda jambo ovu kama hilo. Tutakuwa marafiki ukiniokoa," Simba alisema.
Ngiri alimwonea Simba huruma akasema, "Sifurahii ukihisi uchungu, kiu na kuwa karibu kufa kwa njaa."
Kwa hivyo, alitumia pembe zake akavuta na kumwokoa Simba.
Ngiri akampata rafiki mpya.
Simba alisema, "Asante sana rafiki yangu kwa kuniokoa. Ninaenda kwa familia yangu sasa, kwa heri."
"Nenda salama rafiki yangu," Ngiri alimjibu. Ngiri alifurahi kwamba Simba alikuwa rafiki yake.
"Familia yangu haitamtoroka tena simba," aliwaza.
Simba aliondoka akichechemea kwa unyonge. Alihisi njaa sana.
Aliwaona watoto wa Ngiri wakicheza topeni. Alipowaangalia, alidondokwa na mate akafikiria, "Leo nina bahati."
Simba alimwita Ngiri, rafikiye mpya, "Nilikuwa nimenaswa mtegoni kwa siku nyingi bila chakula. Sina nguvu za kuwinda kwa sasa. Naomba unipatie mmoja wa watoto wako kuwa kifungua kinywa changu?"
Ngiri alishtuka akasema, "Nilikuokoa kutoka mtegoni na sasa unataka kuwala wanangu?"
Simba alimjibu, "Nasikitika rafiki yangu, lakini nina njaa. Elewa kwamba ingawa mimi ni mnyonge sasa mimi ni mwenye nguvu kukuliko wewe." Simba alifungua kinywa chake na kuonyesha meno yake.
"Usiponipatia mmoja wa watoto wako kwa hiari, mwenyewe nitamchukua mmoja," alinguruma.
Ngiri alifahamu kuwa hakuwa na mbio wala nguvu za Simba. Hangeweza kuwalinda wanawe katika vita.
"Nitakupatia mwanangu mmoja baada ya wewe kunionyesha jinsi ulivyonaswa mtegoni. Itanisaidia kumwokoa simba mwingine," Ngiri alisema.
Simba hangeweza kusubiri kumla ngiri mchanga.
Aliuweka mguu wake ndani ya mtego kumwonyesha rafiki yake jinsi alivyonaswa.
"Ui!" Simba alinguruma.
Ngiri alikaza mtego kwenye mguu wa simba akisema, "Aha! Nimekupata. Utakaa mtegoni kwa njaa na kiu tena. Tuone ikiwa meno yako makali na yenye nguvu yatakusaidia sasa."
Mkewe Ngiri aliwaambia wanawe, "Kimbieni! Inueni mikia yenu ili baba yenu awaone mlipo."
Watoto wa Ngiri walikimbia kichakani kwa kasi walivyoweza.
Simba alihisi uchungu akamsihi Ngiri tena amsaidie, "Nitakufanyia lolote utakalo ukiniokoa."
Ngiri hakumwamini Simba. Alimwambia, "La! Sitathubutu, wewe ni muongo! Nitawaonya wanyama wengine pia ili waepuke na ujanja wako."
Ngiri aliwaona watoto wake na mama yao wakikimbia katika mstari mmoja. Waliinua mikia yao ili awaone.
Ngiri alijiunga nao wakatorokea mahali pa usalama.
Hii ndiyo sababu ngiri huinua mikia yao wanapokimbia kuhakikisha usalama wa kila mmoja wao.

