Mwalimu Goso
Adapted from one of George W Bateman’s Zanzibar Tales Versioned by Mitugi Kamundi
Jemma Kahn

Hapo zamani kulikuwa na mwalimu aliyeitwa Goso.

Aliwafundishia wanafunzi chini ya mbuyu badala ya darasani.

1

Siku moja, paa alipanda juu ya mbuyu kuiba matunda.

Alitikisa tawi la mbuyu na tunda moja likamwangukia Mwalimu Goso.

Mwalimu Goso alifariki papo hapo.

2

Watoto walipofika chini ya mti walimpata mwalimu wao akiwa amekufa.

Walihuzunika sana wakataka kujua kilichomuua Mwalimu Goso.

3

Waliushika upepo wa kusini, "Ni wewe uliyeangusha tunda lililomgonga Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Upepo wa kusini ulijibu, "Ningekuwa na nguvu kiasi hicho, ukuta wa matope ungewezaje kunikinga?"

4

Walikwenda kwenye ukuta wa matope, "Ni wewe uliyekinga upepo wa kusini ulioangusha tunda, lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Upepo wa kusini ulijibu, "Ningekuwa na nguvu kiasi hicho, panya angewezaje kutoboa shimo ubavuni mwangu?"

5

Walikwenda kwa panya, "Ni wewe uliyetoboa shimo kwenye ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ulioangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Lakini panya alijibu, "Ningekuwa na nguvu kiasi hicho, paka angewezaje kunila?"

6

Walimwambia paka, "Ni wewe humla panya, anayetoboa shimo kwenye ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ulioangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Lakini paka alijibu, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kufungwa kwa kamba?"

7

Waliiambia Kamba, "Ni wewe humfunga paka, ambaye hula panya anayetoboa shimo ubavuni mwa ukuta wa matope, uliokinga Upepo wa Kusini ambao uliangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Kamba ikasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kukatwa kwa kisu?"

8

Walikiambia kisu, "Ni wewe hukata Kamba, ambayo hufunga Paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa shimo ubavuni mwa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ulioliangusha tunda, ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Kisu kilisema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuchomwa kwa moto?"

9

Basi wakaenda kwa moto, "Ni wewe huchoma Kisu, kinachokata kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa shimo kwenye ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ambao uliangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Moto ulisema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuzimwa na maji?"

10

Waliyaambia maji, "Ni wewe ambaye huzima moto, ambao huchoma kisu, ambacho hukata Kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini ambao uliangusha tunda, ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Lakini maji yakasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kunywewa na ng'ombe?"

11

Walikwenda kwa ng'ombe, "Ni wewe ambaye hunywa maji, ambayo huzima moto, ambao huchoma kisu, ambacho hukata kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ambao uliangusha tunda ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Lakini ng'ombe akasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuumwa na mbung'o?"

12

Basi wakaenda kwa mbung'o, "Ni wewe ambaye humwuma ng'ombe, ambaye hunywa maji, ambayo huzima moto, ambao huchoma kisu, ambacho hukata Kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ambao uliangusha tunda ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Mbung'o akasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuliwa na paa?"

13

Basi wakampata paa, "Ni wewe ambaye hula mbung'o, ambaye humwuma ng'ombe, ambaye hunywa maji, ambayo huzima moto, ambao huchoma Kisu, ambacho hukata kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini ambao uliangusha tunda, ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

14

Paa alishtuka kwamba alikuwa ametambulika. Kwa hivyo, hakuwa na cha kusema.

Kisha watoto wakasema, "Ni wewe uliyeangusha tunda lililomgonga Mwalimu Goso. Ni wewe unayepaswa kuadhibiwa!"

15
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Mwalimu Goso
Author - Adapted from one of George W Bateman’s Zanzibar Tales Versioned by Mitugi Kamundi
Illustration - Jemma Kahn
Language - Kiswahili
Level - Read aloud