

Kama kwenye Malala's Magic Pencil, watoto wa Temeke wametumia penseli ya miujiza kueleza: Unatamani nini katika jamii yako? Nani asaidie ili hilo litimie? Kero gani zinakukwaza na utatatuaje kero hizo? Karibu usome ndoto na sauti zao.
Ninaitwa Ruth. Kitu ninachokitamani katika jamii yangu ni kila mtu awe na nyumba yake kwa sababu watu wanateseka na kunyanyaswa na wenye nyumba wao. Mtu kama hana kodi, anaweza kufukuzwa kwa kudhalilishwa mbele za watu.
Suluhisho
ninatamani serikali iwape watu ajira za kutosha ili wapate fedha za kodi au wajenge nyumba zao wenyewe ili kusiwe na mateso na kudhalilika tena.
Ninaitwa Grace. Ninatamani jamii ya ndoto yangu iwe na ushirikiano kwa kila kitu, pakiwa na misiba, shughuli kama harusi au ugonjwa tusaidiane. Kitu kinachonikwaza ni wizi. Watu wanakuibia, wanakupiga na kukuacha ufe. Inaniumiza sana.
Nitatumia penseli ya miujiza kuondoa wizi na roho mbaya. Ndoto yangu ni kuona watu wakishirikiana kufanya usafi wa mazingira shuleni na nyumbani.
Ninaitwa Aneth. Ninataka jamii yenye ujenzi wa nyumba nyingi za udongo, upandaji miti, na wasichana wasinyimwe haki ya kwenda madrasa. Katika jamii yangu kuna uhaba wa nyumba zenye umeme na madrasa.
Inanikwaza kuona wavulana wanapelekwa madrasa lakini wasichana wanabaki kufanya kazi za nyumbani.
Nimechora nikiwasilisha malalamiko yangu serikalini. Ninatamani serikali itujengee nyumba bora za udongo zenye umeme wa kutosha.
Ninaitwa Lina. Ninatamani kuona jamii inatunza mazingira ya barabarani na sokoni kwa kuchoma na kufukia takataka. Inanikwaza kuona familia nyingi, ikiwemo yangu, hazitoi mgawanyo sawa wa kazi. Wasichana wanachoka sana.
Nitatumia kalamu ya miujiza kuishauri jamii yangu wavulana na wasichana wafanye kazi kwa pamoja kwa usawa bila kujali jinsia ili sote tupate muda wa kupumzika.
Ninaitwa Bahati. Ninatamani jamii inayofuata sheria, mwizi akikamatwa apelekwe polisi apate adhabu. Wizi unaharibu maisha ya watu hasa kwa wale wanaoibiwa wanarudi nyuma kimaisha na wezi wanaweza kufa kwa kupigwa.
Pia inanikwaza kuona wadada wanajiuza mitaani. Ndoto yangu ni kuona watu wanaacha nguo zao wanazofua nje bila kuibiwa, na wasichana wanaenda shule kutimiza malengo yao badala ya kujiuza miili yao ili kupata maisha mazuri.
Ninaitwa Dina. Ninatamani jamii yenye upendo na kuthaminiana, kwenye mchoro wa ndoto yangu mlemavu anasaidiwa kurudi na kupelekwa nyumbani na mwanafunzi mwenzake baada ya kutoka shule.
Miundombinu mibovu inasababisha ajali. Inanikwaza sana kuona barabara mbovu katika makazi yetu. Ombi langu kwa serikali ni kutengeneza miundombinu mizuri kila sehemu ili watu na wanyama wanufaike na kuepuka ajali.
Ninaitwa Rehema. Mchoro wangu ni wa changamoto ya nyumba za kupanga. Wapangaji wanasumbuka na choo, vyumba vidogo, na migogoro ya kulipia umeme. Wapangaji wengine ni wagumu kulipa hela za umeme. Changamoto hizi za nyumba zinanikwaza sana.
Suluhisho
nimechora jamii yenye wajenzi wengi. Ninatamani wanafunzi wasome kwa bidii wawe wajenzi ili kila familia iwe na nyumba yake na kusiwe na kero za kupanga.
Ninaitwa Magreth. Ninatamani jamii inayoshirikiana kufanya usafi wa mazingira yanayotuzunguka. Watu wanatupa taka ovyo na inanichukiza sana. Tusipotunza mazingira tutapata magonjwa kama vile kipindupindu na kuharisha damu.
Nimechora msichana akifanya usafi. Nitaiomba serikali ichukue hatua kali kwa wanaotupa taka ovyo.
Ninaitwa Happiness. Ninatamani wanafunzi waende shule na wazazi wawahudumie watoto wao vizuri. Uchafuzi wa mazingira unaleta kipindupindu na ni kikwazo kikubwa katika jamii yetu ya Temeke.
Kwa kutumia penseli yangu ya miujiza naiona jamii ya ndoto yangu ni safi, imepandwa miti na maua, na kila mtoto msichana na mvulana anapata haki ya elimu.
Ninaitwa Zuwena. Ninatamani maisha mazuri ambayo watoto wanaenda shule na wazazi wanafanya kazi. Katika jamii yetu ya Temeke tuna shida ya maji, mabomba ni machache na watu wanagombania maji yakikatika. Pia wizi wa mabomba unanikwaza.
Mchoro wangu unaonyesha watu wakishirikiana kujenga msikiti. Ninatamani tushirikiane hivyohivyo kuandika na kupeleka hoja serikalini ili tupate mabomba ya maji.
Ninaitwa Kauthar. Inanikwaza kuona watu wanawabagua walemavu na kufanya wizi Temeke. Ninatamani tupendane na kusikilizana kwenye shida na raha. Nitatatua hili kwa kuwashauri watu wasiibe na wasibague walemavu ili tuwe na umoja.
Natamani jamii ya Temeke iwe na maktaba na pia kwa kutumia penseli ya miujiza jamii yangu ya Temeke iwe na ushirikiano na tuwe tunasikilizana kwa kila jambo. Kwenye mchoro huu watoto wakiwa nyumbani wanasoma kwa pamoja bila ubaguzi wowote.
Ninaitwa Loyce. Ninatamani wanafunzi wote waende shule kutimiza malengo yao. Inanikwaza kuona wavuta bangi wakibaka wasichana na kuwaharibia ndoto zao.
Nimechora wanafunzi wakisoma kwa amani. Nitaenda dawati la jinsia kutoa taarifa ili wabakaji wapewe adhabu kali na wasichana walindwe. Jamii ya ndoto yangu ni kuona wanafunzi wote wanasoma na kufikia ndoto zao walizozipanga.
Ninaitwa Mariam. Jamii ya ndoto yangu ni watoto wote, wavulana kwa wasichana, waende shule bila kuzuiwa na wazazi. Inanikwaza kuona watu wanatupa taka sehemu zisizo rasmi na kuharibu mazingira.
Nimechora jamii inayotunza mazingira na kutupa taka sehemu rasmi kwa sababu tukitunza mazingira, mazingira nayo yatatutunza.
Ninaitwa Paulina. Ninatamani jamii yenye mgawanyo sawa wa kazi na ushirikiano katika usafi. Wasichana tunachoka sana na kushindwa kujisomea kwa sababu ya kazi nyingi za nyumbani.
Kutatua changamoto ya mgawanyo wa kazi nitaandika kitabu na kuigiza igizo kuhusu mgawanyo sawa wa kazi. Nimechora jamii ambayo wote tunashirikiana na yenye mgawanyo sawa wa kazi za nyumbani ili kila mmoja apate muda wa kusoma.
Mimi ninaitwa Joyce. Kutupa taka ovyo kunanichosha. Inaleta kipindupindu na kuharisha. Nitatatua hili kwa kuitisha kikao. Nimechora jamii ya ndoto yangu ambayo watu wanafagia na kutupa taka kwenye dustbin ili tuwe na afya njema.
Kwa kutumia penseli ya miujiza nimechora jamii ya ndoto yangu ina mazingira safi na salama ili kuepuka magonjwa, mfano ugonjwa wa kipindupindu na homa ya matumbo.
Mimi ninaitwa Sophia. Jamii ya ndoto yangu ni ya kusaidiana, mfano kumsaidia mwenzako anapopata ajali barabarani. Inanikwaza kuona watu wazima wakibeba mizigo mizito bila kusaidiwa na watoto wao au wanafunzi wao.
Nimechora watoto watiifu wakisaidia watu wakubwa kubeba mizigo. Hiyo ndiyo jamii yenye adabu niliyoichora na penseli ya miujiza. Vitendo hivi vinaleta heshima katika jamii na kuwa na sifa nzuri.
Ninaitwa Stella. Sitaki jamii yangu iwe maskini, jamii ya ndoto yangu nataka iwe na nyumba nzuri, ajira, na elimu kwa wote. Inaniumiza kuona watu wanaokota machupa ili wauze ndio wale. Ninatamani watu wasome ili wasiteseke.
Nimechora jamii yenye shule na ofisi. Kwa kutumia penseli ya miujiza nimechora watu waliopata ajira na wanaishi maisha mazuri. Hamna vibaka kwa sababu kila mtu anafanya kazi. Wanafunzi wanaenda shule na familia zinaishi kwa furaha.
Ninaitwa Dorcas. Natamani jamii ya ndoto yangu isiwe na ubaguzi wa msichana au mvulana. Tusibague msichana kilema au mwenye ulemavu wa ngozi. Wote wasalimiane na kucheza rede pamoja. Majirani zangu huwacheka walemavu wakipita mtaani kwetu.
Hilo linanikwaza sana. Nimechora jamii ya ndoto yangu ambayo watu wanapendana na hawabaguani. Nitaenda kwa majirani zangu na kuwaambia kuwa walemavu wana haki kama watu wengine wasio na ulemavu kwenye jamii yetu na tusiwacheke.
Ninaitwa Angel. Ninatamani shule zijengwe, miti ipandwe, na mabomba ya maji yawepo. Inanikwaza kuona wavulana wakivuta bangi na kunywa pombe. Jamii ya ndoto yangu nataka watoto wote wasichana na wavulana waende shule wakasome kwa bidii.
Penseli yangu ya miujiza imechora wasichana na wavulana wakienda shule kupata elimu na baadae kuwasaidia wazazi wao.
Mimi ninaitwa Kamila. Ninatamani watu wasiharibu miti wala kupoteza maji kwa kuacha mabomba wazi. Takataka na upotezaji wa maji ni kikwazo kikubwa kwenye jamii yetu. Ninatamani baba yangu (ambaye ni mjumbe) anisaidie kukomesha hili.
Kwa kutumia penseli ya miujiza mchoro wangu unaonyesha watu wakishirikiana kufanya kazi na hakuna anayetupa taka ovyo wala kuacha mabomba wazi.
Ninaitwa Halima. Ninataka jamii ya ndoto yangu iwe inavaa stara na isivae mavazi ya uchi si mazuri kwa jamii.
Mimi Mudh-dalifa. Nimechora mazingira yanayopendeza na kuvutia. Ukeketaji wa wasichana unanikwaza sana Temeke. Natamani ukomeshwe. Kalamu ya maajabu inaonyesha wasichana hawakeketwi bali wanalindwa na mazingira yanapambwa kwa miti na maua.
Mimi ninaitwa Leyla. Inaniumiza kuona unyanyasaji wa kijinsia na akina mama wanaochoma watoto wao moto kwa sababu ya kazi za nyumbani. Kalamu yangu ya miujiza itafanya kila msichana aende shule bila hofu ya kubakwa wala kuteswa nyumbani.
Mimi ninaitwa Faima. Inanikwaza kuona ndugu akilewa na kumpiga mwenzake bila sababu. Ninatamani ndoto yangu ya familia yenye amani itimie. Nimechora jamii yenye ushirikiano; mmoja anafagia na mwingine anapanda maua na miti.
Mimi ninaitwa Wadhiat. Mama haniruhusu kwenda shule, ananiambia nibaki nyumbani kufanya kazi wakati wenzangu wanaenda.
Nimechora mtoto analia akichungulia dirishani. Ombi langu kwa wazazi ni kuniruhusu nitimize ndoto zangu shuleni.
Mimi ninaitwa Swalhati. Inanikwaza kuona vijana wanaharibika kwa kuvuta bangi. Nimechora vijana waliokuwa wanavuta bangi sasa wameacha na wanafanya kazi za maendeleo kwa ushirikiano.

