LUGHA ZA MAISHA YETU
Wasichana wa Shule ya Msingi Twiga
Deonarda Damian

Unajua lugha zipi? Unazitumia wapi, ukiwa na nani na kwa malengo gani? Unatarajia kutumia lugha zipi mbeleni?
Wasichana wa darasa la 5 wa Klabu ya Hadithi Zetu wa Shule ya Msingi Twiga, iliyoko Manispaa ya Temeke, walichunguza maswali haya kwa kina. Walichora ramani kuonesha matumizi ya lugha mbalimbali katika maisha yao wakitumia rangi tofauti kuwakilisha lugha tofauti. Walijadili, kuandika na kufundishana kuhusiana na lugha zao hatimaye kuunda kitabu hiki.

1

Ninaitwa Ashura. Ninatumia lugha tatu: Kiswahili, Kiingereza na Kindengereko. Kiswahili nimefunzwa na mwalimu pamoja na mama, Kiingereza nimfunzwa na mwalimu. Kindengereko nilijifunza kutoka kwa bibi yangu. Pia, nimejifunza Kiarabu madrasa.

Natumia lugha hizi katika mazingira tofauti: Kiswahili shuleni na nyumbani, Kiingereza darasani au ninapojisomea nyumbani.

Mbeleni nitakuwa daktari na kufanya kazi China, nikiwa nazungumza Kichina.

2

Mimi ni Asma. Ninajua lugha tatu: Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu. Kiswahili nimefundishwa na mamangu, Kiingereza na Mwalimu, na Kiarabu nimefundishwa na Ostadhi.

Ninatumia lugha hizi katika mazingira tofauti: Kiswahili nikiwa nyumbani, Kiingereza nikiwa shuleni, na Kiarabu nikiwa msikitini na waislamu wenzangu. Ninatumia lugha ya Kiswahili kujitambulisha, kusoma na kuzungumza. Nitatumia Kiingereza endapo nitakuwa Uingereza.

3

Mimi ni Farhya. Ninajua Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu. Kiswahili hukitumia shuleni, Kiingereza nikiwa darasani na Kiarabu nikiwa madrasa. Kila lugha ina umuhimu katika mazingira tofauti.

Nitajifunza lugha ya Kichina kwani ninategemea kuwa daktari na kufanya kazi ya utibabu China na Uingereza.

4

Ninaitwa Jamila. Ninajua lugha tatu: Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu. Ninatumia Kiswahili na Kiingereza shuleni, na Kiarabu nikiwa madrasa pamoja na Ostadhi. Lugha hizi ni muhimu kwangu kwa sababu zinaniwezesha kuelimisha na kuwasiliana na watu katika jamii.

Nina ndoto ya kwenda nchi za nje ambako nitatumia zaidi lugha ya Kiingereza.

5

Ninaitwa Josephina. Ninajua Kiswahili, Kiha na Kiingereza. Nyumbani natumia Kiha na Kiswahili, na shuleni Kiingereza. Lugha hizi nimefundishwa na wazazi, bibi na walimu.

Mbeleni nataka kujua Kichina ili nikitumie kwa mawasiliano nikiwa China na Kigogo ili nikienda sehemu kama Dodoma niweze kuwasiliana vizuri na wenzangu.

6

Ninaitwa Khairhati. Ninajua Kiswahili, Kiingereza na Kisambaa. Ninatumia lugha hizi mahala tofauti: nyumbani na kwa bibi natumia Kisambaa, shuleni Kiingereza, na Kiswahili kila mahali. Lugha hizi ni muhimu kunisaidia kuelewa masomo na kuwasiliana na familia.

Mbeleni nataka kujua Kijapani, Kiarabu na Kihindi kwa ajili ya kazi na safari. Nitajifunza lugha hizi kupitia tafiti.

7

Mimi ni Khyrath. Ninajua Kiswahili, Kipemba, Kiingereza na Kiarabu. Natumia Kiswahili na familia, Kipemba nikiwa Pemba, Kiingereza darasani na Kiarabu madrasa. Natumia lugha hizi kuwasiliana. Nimejifunza lugha hizi kutoka kwa mama, Mwalimu na Ostadhi.

Mbeleni nataka kujua Kichina, Kihindi na Kijapani ili nisiwe na aibu kuongea na wenzangu.

8

Ninaitwa Mwanamosi. Ninajua lugha tatu: Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu. Ninatumia Kiswahili nyumbani na mtaani, Kiingereza shuleni na Kiarabu nikiwa madrasa. Kiingereza ni muhimu kwa ajili ya mawasiliano nikiwa nje ya nchi.

Mbeleni nataka kujua Kichina na Kinyasa ili nizitumie kuandika na kusoma vitabu.

9

Ninaitwa Rujaina. Ninajua Kiswahili na Kiingereza. Ninatumia Kiswahili nyumbani na Kiingereza darasani wakati wa somo la Kiingereza. Kiswahili ni muhimu kwangu kwa kuwa ni lugha ya taifa, na Kiingereza kitakuwa na faida nitakapokuwa mkubwa. Lugha hizi nimejifunza kutoka kwa ndugu zangu na mwalimu.

Baadaye, natamani kujifunza Kituruki, Kiarabu, Kichina na Kinyamwezi kwa ajili ya mawasiliano katika kazi zangu za udaktari.

10

Ninaitwa Safi. Ninajua lugha tatu: Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu. Kiswahili amenifundisha mama, Kiingereza nimefundishwa na Mwalimu shuleni, na Kiarabu amenifundisha Ostadhi. Ninategemea kutumia Kiingereza na Kiarabu kwa mawasiliano nikiwa nafanya kazi katika nchi za Uingereza na Uarabuni.

Mbeleni nataka kujua Kichina, Kihindi, Kifaransa na Kirumi ili niwasiliane na marafiki zangu na wafanyakazi wenzangu nikiwa katika nchi hizo.

11

Mimi ni Sania. Ninajua lugha tatu: Kiswahili, Kiingereza na Kipemba. Ninatumia Kiswahili na Kiingereza shuleni na nyumbani, hasa nikiwa na baba anayezungumza Kiingereza. Kipemba hutumika nyumbani na mama na ndugu zangu. Kiswahili ndiyo lugha yangu kuu ya mawasiliano.

Baadaye natamani kujifunza Kichina na Kihindi ili niweze kuwasiliana vizuri nikiwa huko kazini.

12

Ninaitwa Yusra. Ninajua lugha tatu: Kiswahili, Kiingereza na Kindengereko. Ninatumia Kiswahili kuhadithiana na ndugu zangu. Ninatumia Kiingereza darasani wakati wa somo la Kiingereza. Ninatumia Kindengereko ujombani nikiwa na bibi na wajomba.

Lugha zote ni muhimu kwangu kwa mawasiliano katika maeneo na watu tofauti lakini napenda zaidi Kindengereko.

13

Ninaitwa Zaituni. Ninajua lugha ya Kiswahili, Kiingereza na Kisambaa. Lugha hizi ninazitumia kila moja kulingana na mazingira yake.
Nyumbani hutumia Kiswahili, shuleni Kiswahili na Kiingereza, madrasa Kiarabu. Vilevile nitatumia Kiingereza kuwasiliana na wageni kutoka nchi za nje wakitutembelea.

14
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
LUGHA ZA MAISHA YETU
Author - Wasichana wa Shule ya Msingi Twiga
Illustration - Deonarda Damian, Klabu Ya Hadithi Zetu, Asma Mohamed Mohamed, Farahya Issa Issa, Jamila Said Miuki, Khairath Hemed Hemed, Khairath Muniri Abdalah, Mwanamosi Yahya Semu, Rujaina Mwalami Ally, Safi George Kimondo, Yusra Mohamed Mohamed, Zaituni Idd Shekalage, Wasichana Wa Twiga, Ashura Al- Hati, Josephina Ayoub Yete, Sania Mohamed Nasoro
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs