Changamoto ya Naisam
Loveness Joseph Ngowi
Shule Ya Msingi ya Mwasi Kaskazini

Naisam alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nariver. Alikuwa na umri wa miaka kumi na tatu. Aliishi katika Kijiji cha Songambele.

Naisam aliishi na bibi, babu, na baba. Mama yake Naisam alimwacha tangu akiwa na umri wa miaka mitatu. Naisam yeye hakumjua mama yake.

1

Naisam yeye alimzoea bibi na babu. Hakumzoea baba kwa sababu baba alikuwa kazini.

Naisam alikuwa na bidii sana katika masomo yote. Nyumbani alikuwa na bidii sana kwenye kazi.
Naisam kila siku usiku alikuwa anapiga hadithi na bibi na babu mpaka walipokuwa wanasikia usingizi wakilala.

Naisam alikuwa karibu sana na shule. Kwake ilikuwa rahisi sana kwenda shule. Naisam yeye tangu akiwa mdogo alipenda kuwa daktari wa kutibu binadamu.

2

Baba yake Naisam alikuwa anafanya kazi ya kuchomelea, kwa mfano magrili, milango, madirisha, n.k. Baba yake Naisam akawa anachelewa kurudi nyumbani. Na alikuwa anarudi akiwa amelewa usiku. Hakupata tena muda wa kuongea na mtoto wake kwa sababu alikuwa anarudi usiku na kukuta tayari Naisam amelala.

3

Naisam alikuwa akitoka shule anafua nguo, anaokota kuni, anabandika maji ya kuoga, anaenda kuoga, ndipo wanakula na wanahadithiana hadithi na bibi na babu.

Lakini kadri siku zilivyoenda, macho ya babu na bibi yakawa vigumu kuona mbali, miguu ilianza kuuma, na wakaanza kusumbuliwa na magonjwa. Baada ya mwezi mmoja, babu alifariki. Bibi na Naisam walikuwa na huzuni.

Na miaka miwili ilivyopita, bibi na yeye pia alifariki. Wakamzika. Baada ya kuzika, Matanga yalifanyika.

4

Baada ya mazishi, baba yake Naisam alikuwa anamlea mwanaye peke yake. Naisam alipokuwa na baba yake, akamwuliza, "Baba mbona mama yangu simjui na wala sijawahi kumwona?" Baba yake aliguna.

Naisam akamwambia, "Mbona unaguna? Mama yangu yuko hai? Na kama yuko hai, yuko wapi?" Baba akajibu, "Mama yako alikuacha ukiwa mdogo kwa sababu baada ya mimi kuchelewa kurudi nyumbani nikakukuta hamna mtu uko mwenyewe. Ndio ukaja kuishi na bibi." Naisam alilia kwa uchungu aliposikia hivyo.

5

Siku moja baadaye, baba yake Naisam aliwahi sana kutoka kazini na kurudi nyumbani. Naisam alimpokea baba yake kwa furaha. Lakini baba yake hakuwa na furaha. "Baba mbona hauna furaha?" Naisam akamwuliza. Baba akajibu, "Nimechoka tu." Lakini Naisam hakurizika na jibu la baba yake.

Baba yake Naisam alikuwa amekaa sebuleni na Naisam. Baba yake Naisam alimwangalia sana Naisam. Naisam alimuuliza baba yake, "Kuna nini?" Baba hakujibu. Alikaa kimya dakika tano.

6

Baba yake Naisam alisema, "Nataka nikuozeshe kwa Anuary." Naisam akauliza, "Anuary ndiye nani?" Baba yake akajibu, "Ni miongoni mwa matajiri wa kijiji chetu cha Songambele."

Naisam akasema kwa huzuni, "Kwani baba mimi ni mwanafunzi na bado sijafikia kuolewa. Mimi sintakubali. Vinginevyo baba mimi nitakushtaki." Baba akamwambia kwa hasira, "Nataka Anuary akuoe. Wewe hutaki kuishi maisha mazuri?"

7

Naisam akajibu, "Maisha mazuri ninataka kuishi lakini lazima na mimi nifanye kazi. Siwezi kuishi majumba mazuri ya kitajiri ambayo sijatolea jasho." Lakini baba hakuelewa.

Naisam aliona kwamba anasikia usingizi kwa hiyo alitaka kumaliza mazungumzo hayo. Alisema, "Sawa baba, nimekubali." Baba yake alifurahi kusikia hayo. Naisam alimwaga baba yake.

8

Ilipofika muda wa saa mbili, Naisam alianza kupanga nguo zake. Mpaka saa tatu alikuwa amejiandaa vizuri. Alivaa nguo kubwa za kipindi cha baridi. Naisam aliondoka kuelekea mlangoni. Akatoka nje akiwa ananyata.

Naisam akaenda mbali sana na nyumbani. Alichoka sana. Akapumzika kwenye mti. Alipitiwa na usingizi. Akalala na kukoroma.

9

Mama mmoja alikuwa akielekea nyumbani kwake. Alishangaa sana kumwona mtu amelala chini ya mti usiku wa saa tano. Aliokota fimbo na kumgusa nayo. Naisam alishtuka. Alimsalimia, "Shikamoo." Yule mama akajibu, "Marahaba. Nini shida?" Akamjibu, "Kwa ufupi, hadithi yangu ni ndefu sana. Naomba unisaidie. Nitakuelezea."

Wakafika nyumbani. Wakalala kwa sababu walikuwa wamechoka sana.

10

Asubuhi baada ya kifungua kinywa, mama yule alitaka kujua kuhusu Naisam. Naisam alimwelezea kuanzia alivyoachwa na mama yake na kuishi na bibi yake na hadi ilivyotokea alipomkuta pale.

Naisam akaishi na yule mama na pia aliendelea na shule huko.

11

Siku moja, Naisam alipokuwa akifanya usafi, aliona picha ya watu watano. Alipigwa na butwa na kushangaa na kujiuliza maswali.

Kwenye ile picha, alishangaa kumuona bibi yake, babu yake, baba yake, na mama huyo anayeishi naye. Na mtoto. Aliona mtoto alikuwa na alama nyeusi shingoni. Na Naisam pia alikuwa na alama shingoni.

12

Kadri siku zilivyoenda, alipata hisia ya kutaka kujua. Siku moja, alipatwa sana na shauku. Akasema, "Lazima niulize kwa sababu wahenga walisema kuuliza si ujinga." Kwa hiyo alimwuliza yule mama.

Yule mama alijibu, "Huyo mtoto ni wangu. Nilimwacha tangu akiwa na miaka mitatu." Naisam alijibu, "Mimi pia niliachwa na mama yangu nikiwa na miaka mitatu." Naisam alipatwa na hisia kuwa huyo ni mama yake. Yule mama pia alijua kuwa huyo ni mwanae. Walikumbatiana kwa furaha.

13

Naisam aliendelea na shule. Alifanya mitihani ya Form Four. Alifaulu. Aliendelea na Form Five na Form Six. Akafaulu tena. Akaenda chuo kikuu. Akapata kazi yake ya kuwa daktari.

Baada ya miaka miwili, aliolewa na kuishi kwake. Alibarikiwa kupata mtoto wa kike. Aliamua kumtafuta baba yake na kumkutanisha na mjukuu wake. Babake alimwomba Naisam msamaha kwa kutaka kumwozesha kabla hajamaliza shule. Naisam alimsamehe.

14

Kila alipopata likizo, Naisam alienda kumsalimia mama yake, na baba yake pia. Likizo moja, alipoenda kwa mama yake, akamwambia, "Nataka kukukutanisha na mtu muhimu." Mama yake alikubali.

Naisam akampeleka mama yake na kumkutanisha na baba yake. Naisam alifanikiwa kuwapatanisha. Wakapendana tena. Mama na baba yake Naisam waliishi tena pamoja.

15

Siku moja, Naisam aliwakutanisha wazazi wake, mume wake, na mtoto wake. Walikula na kunywa kwa furaha. Walifurahi kwani Naisam ndiye alikuwa ni mwenye busara.

Waliishi kwa furaha na upendo.

16
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Changamoto ya Naisam
Author - Loveness Joseph Ngowi
Illustration - Shule Ya Msingi ya Mwasi Kaskazini
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs