

Mimi ninaitwa Ester. Mimi nilizaliwa katika hospitali iitwayo Muhimbili katika Jiji la Dar es Salaam. Nililelewa Dar es Salaam.
Nilipofikisha miaka mitatu, nikaanza chekechea. Nikasoma chekechea katika shule ya awali ya Dola English Medium mpaka nilipomaliza. Nilisoma hapo na nilijitahidi sana kwenye masomo.
Mwalimu alikuwa akinipongeza na kunipa zawadi. Nilikuwa mtu wa kujisomea sana na baba yangu alinipa zawadi. Alikuwa akinifundisha na alikuwa akiniambia, "Soma mwanangu ili uweze kunisaidia." Mama pia alisema hivyo hivyo.
Baada ya kumaliza awali, niliingia darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ya Maendeleo nikiwa huko Dar es Salaam kwa mama. Nilisoma Shule ya Maendeleo kwa mwaka mmoja na nusu.
Baada ya hapo, bibi aliniomba nije kukaa naye. Nami pia nilifurahi sana kwenda kwa bibi kwa sababu kule nilipokuwa, ufaulu wangu ulishuka sana. Lakini sikukata tamaa na pia baba yangu hakukata tamaa kunifundisha.
Baba aliendelea kunielekeza cha kufanya. Pia mama alisema hivyo. Niliongeza bidii zaidi na zaidi. Baada ya hapo, baba alinipakiza kwenye gari. Nikaja na mama kwa bibi. Mama yangu aliniombea uhamisho na kunileta huku shuleni Moshi kwa bibi.
Nilifurahi sana sana. Pia wakanileta kwa bibi na pia nilifika shuleni. Walimu walinipokea vizuri. Mama yangu aliniambia, "Soma kwa bidii na upambane vizuri." Nilisema, "Sawa mama." Nilifika shuleni. Nikapewa kitabu cha kusoma. Nikasoma.
Baada ya hapo, niliingia darasani na kuendelea na masomo. Wanafunzi wenzangu walinikaribisha vizuri na walinipa ushirikiano katika kusoma darasani. Nilifurahi sana.
Wenzangu walinionesha mazingira ya shule. Nilicheza nao na kunywa nao uji.
Lakini mama yangu alipofunga safari kurudi Dar es Salaam, nililia na kusema, "Mama, mimi nimeshakuzoea. Usiondoke!" Nililia sana.
Lakini mama aliniambia, "Mwanangu, ningebaki lakini nimeshakata tiketi kwa ajili ya kuondoka."
Nililia na kuhuzunika sana. Lakini mama yangu alinifuta machozi na kuniambia, "Usilie. Nitakuja kukusalimia vipindi vyote vya likizo."
Niliendelea na masomo mpaka nilipofika darasa la tatu. Ndugu yangu aitwaye Jesca alikuja kwenye msiba wa babu mzaa baba. Tulikwenda kuzika na tukamaliza salama. Bibi aliomba tukae pamoja.
Baba na mama yake Jesca walikubali. Jesca akaandikishwa shuleni. Na wakachukua uhamisho kutoka Dar es Salaam kumleta huku. Tuliendelea kusoma na tukasoma kwa bidii mpaka tumefika darasa la sita. Tunaendelea kuishi pamoja na kusoma pamoja.

