

Katika Kijiji kimoja kiitwacho Funga Moyo, palikuwa na mwanamme mmoja aliyeitwa Steve.
Steve alikuwa na mke na watoto wawili. Alikuwa mvuvi wa samaki.
Steve alipopata pesa aliwalipia watoto wake karo ya shule.
Zingine alinunua chakula. Hata hivyo, pesa zake hazikutosha mahitaji yote ya nyumbani.
Siku moja alienda mtoni kuvua samaki kama desturi yake. Kando ya mto palikuwa na mamba lakini Steve hakumuona.
Ghafla, yule mamba akamrukia Steve na kummeza.
Alipokuwa tumboni mwa mamba alikuwa bado hajapoteza fahamu. Aliona kitu kilichometameta.
Alikichukua na baadaye aligundua kwamba ilikuwa dhahabu.
Steve alianza kumpiga mateke akitaka kutoka. Mamba alihisi maumivu akamtapika Steve.
Steve alibahatika kutoka na ile dhahabu. Alichukua ndoo yake ya samaki akaenda nyumbani.
Steve alikuwa na furaha tele alipokaribia nyumbani.
Mkewe alipoona tabasamu yake, alimwuuliza, "Mbona umekawia sana, na tabasamu ni ya nini?"
Steve alimjibu mukewe, "Hebu nikueleze kilichotokea huko mtoni."
Akamuonyesha ile dhahabu.
Walienda kuiuza na kupata pesa.
Walijenga nyumba kubwa na kununua gari. Wakawa miongoni mwa watu tajiri Kijijini.

