Ndoto Zetu (Kitabu #2)
Wasichana wa Shule ya Msingi ya Mwasi Kaskazini
Klabu Ya Hadithi Zetu

Sisi ni wasichana wa darasa la 5 na la 6 kutoka Shule ya Msingi ya Mwasi Kaskazini. Tumeandaa kitabu hiki katika klabu yetu ya Hadithi Zetu mwaka wa 2025.

Tunatumaini ndoto zetu zitawatia moyo watu wengine kuwa na ndoto kubwa maishani na kwenye jamii zao.

1

Mimi ni Avemaria. Ndoto yangu ni kuwa mwimbaji wa nyimbo za Mungu. Watu wafurahie, kuburudika, na kuja kuzirushia kwenye mitandao. Wazazi watafurahi kwa kipaji changu cha kuimba.

Nitafanya shughuli za ufugaji wa kuku ili nipate mayai, nyama, na niwauze nipate hela. Nitawanunulia pumba na uduvi

2

ili wapate virutubisho na wawe wanono.
Nitawajengea wazazi wangu nyumba ili waweze kufurahi. Nitawanunulia gari na pikipiki.

Ninataka kusoma mpaka chuo kikuu. Nitakuwa ninaongea lugha za Kiswahili, Kiingereza, na Kichaga. Mfano jina langu ni Ave. My name is Ave. Shimboni shavo.

3

Ninaitwa Saraphina. Nina ndoto ya kuwa nesi ili kutibu wagonjwa. Nina kipaji cha kuwachekesha watu wakiwa na huzuni.

Ninataka kuishi Rombo Mkuu kwa bibi na babu. Ninapenda jinsi wanavyoongea lugha yao. Rombo panavutia kwa jinsi mimea yao ilivyo.
Nitakuwa ninaongea Kichaga, Kirombo,

4

na Kiswahili, na kutambua lugha nyingine kama Kiingereza na Kihehe.

Ninataka kuwa na familia yenye baba, mama, na mtoto mmoja au wawili ili kunisaidia na kufuatilia ndoto za mamaye. Nina ndoto ya kuwashauri jamii yangu ijue kuwa kipaji ni kizuri sana na kinawasaidia watu wengi.

5

Ninaitwa Angela. Nina ndoto ya kuwa mwanasheria ili niweze kulinda sheria za nchi na kutetea haki za watu.

Ninataka kusoma hadi chuo kikuu ili nifanikishe elimu yangu. Ninataka watu waziheshimu sheria zake na kutetea haki za binadamu.

Ninataka kulinda misitu na watu

6

wanaokata miti ovyo waache kukata miti ovyo.

Ninataka kuishi Dar es Salaam kwa sababu nitakuwa ninafanya kazi yangu huko. Nitakuwa naongea Kiingereza, Kiswahili, Kichaga, Kichina, Kinyakyusa, Kimaasai, na Kikorea kwa sababu ninataka kufanya kazi yangu sehemu mbalimbali.

7

Mimi ni Consolata. Ninataka kuwa daktari. Nitatibu wagonjwa na kuwapa dawa muhimu. Pia nitawasaidia wazazi kazi ndogondogo. Nataka kufikia chuo kikuu na kuishi Mwasi Kaskazini au Dar es Salaam. Nimewahi kwenda kumsalimia shangazi huko Dar es Salaam.
Nataka familia nzuri na yenye utii.

8

Ninaitwa Janeth. Ndoto yangu ni kuwa msusi. Nataka kufikia mpaka chuo cha ususi. Ninataka kuishi mjini. Ninataka watu wajue kipaji changu cha kusuka. Nitakikuza sana. Nitafundisha jamii wajue kuwa kipaji ni muhimu.

Ninataka kuwa na familia ya watoto

9

wenye nidhamu ya hali ya juu na heshima kwa walimu na wazazi na hata jamii kwa sababu mtoto akiwa na tabia mbaya hataweza kufikia ndoto zake. Nina ndoto ya kuwaeleza jamii wajue kipaji changu na ndoto zangu kuhusu ususi. Mungu anibariki. Thank you.

10

Ninaitwa Febronia. Nina ndoto ya kuwa mwalimu. Nitafundisha watu kwa manufaa ya jamii. Watakuja kunisaidia mbeleni. Nataka jamii iwe na hali nzuri na watu wawe wachapakazi na wawe wanasaidiana.

Nitafundisha Shule ya Msingi Mwasi Kaskazini na hata Kishumundu.
Ninataka kufanya

11

shughuli za kulima, kuosha vyombo na kupika ili nipate fedha ya kununua chakula na nguo zangu na kuwasaidia wengine kama wagonjwa na vipofu. Nitakuwa naongea lugha nyingi kama Kimaasai, Kichaga, Kiswahili, na English. Kusalimia kwa Kimaasai ni Takwenya. Kuitikia ni Iko.

12

Ninaitwa Sharoni. Ninataka kuwa mhasibu ili kuwahesabia wananchi fedha zao. Nitaongea Kiswahili, Kiingereza, Kichaga, Kikorea, Kimaasai, Kifaransa, Kikuria. Nitawasaidia wazee, walemavu, na albino.

Familia yangu itakuwa na ushirikiano. Tukigombana tuweze kupatana kwa kubadilishana mawazo.

13

Ninaitwa Glory. Ndoto yangu ni kuwa daktari ili niwahudumie wagonjwa. Ninataka kufuga kuku kwa ajili ya mayai, nyama na fedha.

Nataka kusoma hadi chuo kikuu na kuishi kwenye nyumba ya ghorofa. Ninataka kuongea Kiswahili kwa sababu unaweza kukitumia na watu wengi sana katika jamii.

14

Ninaitwa Mourine. Ndoto yangu ni kuwa daktari wa mifugo katika jamii ya Mwasi Kaskazini. Nimekuwa na ndoto hii tangu darasa la kwanza. Nataka kuishi Dar es Salaam ili kuendeleza kipaji changu. Nitasoma hadi chuo kikuu na kusomea udaktari wa mifugo.

Nitaongea lugha ya Kiswahili katika

15

jamii yetu ya Mwasi Kaskazini. Nataka kuwa na familia yenye utulivu, upole, na ufukara. Nitakuwa na watoto wawili.

Vikwazo vinavyosababisha wasichana wasitimize ndoto zao ni kama kufanyishwa kazi, kuteswa, kulazimishwa kuolewa kabla ya kufikia umri wake na kushindwa kufikia malengo yao.

16

Ninaitwa Aneth. Ninataka kuwa daktari kwa sababu kuna watu wanaoteseka kwa kuumwa. Nataka niwatibu kabisa wapone, wasiwe na maumivu tena. Wachio kama watu wengine ambao hawana matatizo.

Mabadiliko ninayotaka kuleta ni kufanya jamii yetu iwe na furaha, wasiumwe, waishi kwa amani. Nataka kuishi

17

huku Mwasi Kaskazini ili niwaelimishe kuhusu ndoto zao.

Napenda sana kujua lugha nyingi. Popote nitakapokwenda nataka nijue lugha yao, kwa mfano Wamaasai, Wahehe, n.k. Natamani sana niende huko kwao nikajifunze lugha zao. Nataka kulea watoto vizuri bila ubaguzi kati ya wavulana na wasichana.

18

Ninaitwa Catherine. Nina ndoto ya kuwa sista. Nataka kanisa lijae na kumsifu mungu.

Na ninataka kuwashauri watu kama wakunywa gongo, wavuta sigara, na watafuna mirungi waache hizo tabia.

19
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Ndoto Zetu (Kitabu #2)
Author - Wasichana wa Shule ya Msingi ya Mwasi Kaskazini
Illustration - Klabu Ya Hadithi Zetu
Language - Kiswahili
Level - First paragraphs