

Hapo zamani za kale, palikuwa na wasichana wawili walioitwa Judi na Hepi. Walipenda mazingira na mazingira yaliwapenda. Waliishi kwenye kijiji chenye milima na mabonde na maua ya waridi.
Kulikuwa na mashamba ya maharagwe na mahindi na wanakijiji walitegemea mashamba hayo kwa kupata chakula chao. Kulikuwa na chemchemi, mifereji, na mabomba ambayo wanakijiji walitegemea maji hayo kwa mahitaji yao yote.
Judi na Hepi waliyapenda mazingira yao na waliishi kiusafi. Lakini waliona watu wakikata miti ovyo. Pia watu walitupa matakataka ovyo, kwa mfano plastiki na chupa, na kujisaidia hadi kwenye vyanzo vya maji.
Watu walitumia yale maji kunywa na kupikia. Watu walipatwa na magonjwa, mpaka watu wengine walikufa.
Wasichana hao wawili walichukizwa na vitendo hivyo. Walipanga mkutano. Waliwaita watu wote kwenye kijiji chao na kuwapa ushauri. Waliwaambia wasiharibu mazingira. Lakini wanakijiji walibisha.
Wasichana hao walipata changamoto nyingi. Wengine waliwatukana kwa kusema, "Pumbavu!" "Washenzi!" Watu wengine waliwadhalilisha kwa kusema, "Mnatudanganya tuchunge mazingira!" Watu wengine waliwacheka kwa kusema, "Wajinga nyie!"
Judi na Hepi waliendelea kuwapa ushauri wasitupe matakataka ovyo. Pamoja na kwamba walikutana na upingamizi, Judi na Hepi hawakukata tamaa.
Siku moja, Judi na Hepi walisimama tena mbele ya wanakijiji wenzao na kuwapa ushauri. Lakini watu hao waliguna. Walishauri wasitupe takataka ili wasipatwe na magonjwa mbalimbali, kwa mfano kutapika na kipindupindu. Watunze mazingira ili kutunza vizazi vijavyo.
Watu wengine walianza kuelewa kwamba wakitupa matakataka watapatwa na magonjwa. Baadhi ya watu walikataa kwa kusema ni uongo. Wale wasichana walifurahi kwa wale waliokubali.
Lakini Hepi akaamua kutoa ushauri zaidi ili wasipatwe na magonjwa. Watu wote walikubali na kushangilia. Walianza kutunza mazingira kwa kufanya vitu vifuatavyo: kufagia, kuokota takataka, kutokuchoma miti ovyo, na kadhalika.
Walianza kuchunga mazingira kwa umakini. Pia wakamteua mtu maalumu wa kulinda mazingira. Akimwona mtu akitupa takataka, amkamate ili wanakijiji wamwonye.
Baada ya hapo, maisha ya wanakijiji yalibadilika na kuwa masafi. Judi na Hepi waliishi kwa furaha na kuendelea kuwasisitiza wanakijiji wasitupe takataka ovyo.

