

Linda aliishi kijiji cha Songambele.
Aliishi na mama wa kambo na baba yake mzazi, baada ya mama yake kupotea.
Siku moja, baba yake alisema anasafiri kikazi. Uso wa Linda ulijawa na huzuni lakini baba yake hakufahamu.
Baba yake alipopanda tu kwenye gari, Mama wa kambo alimvuta na kumwambia, "Unatakiwa uoshe vyombo, udeki, upike, ufagie, kisha ukaangue matunda msituni." Linda akamwambia, "Ninahitaji kusoma, Mama." Linda alijua kuwa akienda shule, atawaelezea walimu, na walimu watamsaidia.
Mama wa kambo aliposikia vile, alimkemea kisha akampiga. Akamwambia, "Fanya nilichosema. Usipofanya, nitakupiga." Linda akaenda kutoa vyombo nje na kuosha.
Alimaliza kwa kuchelewa. Mama yule alimpiga na kumwambia, "Nina njaa. Ninahitaji kula. Fanya haraka."
Linda alideki. Alijua kuwa akimaliza kwa kuchelewa atapigwa kwa hiyo alifanya haraka. Alimaliza kwa haraka.
Kisha Linda akapika chakula. Kilipoiva, alipakua kwenye hotipoti kisha akapeleka mezani. Halafu akaandaa vyombo vya mezani. Alipotaka kukaa ale, mama yule alimpiga. Akamwambia, "Nenda kaangue matunda. Hutakiwi kula kwani mimi ni mama yako, unatakiwa kunitii."
Linda alichukua mfuko na fimbo. Akaenda msituni. Alisikia sauti ya wanyama kutoka upande wa kushoto na huko ndiko kwenye matunda. Aliogopa sana.
Alirudi nyumbani akiwa na njaa na hana matunda. Alipigwa na kisha akaambiwa aondoke. Aliondoka akiwa na njaa. Alienda kwa shangazi yake.
Shangazi yake alimlea na kumtunza. Pia Linda alisomeshwa na shangazi yake. Alifurahi sana. Kadri siku zilivyoenda, Linda alimkumbuka baba yake zaidi na zaidi.
Linda alipokuwa darasa la kwanza, baba yake alirudi. Alipofika nyumbani, alimwuliza yule mama, "Linda yuko wapi?" Yule mama hakujibu chochote. Baba Linda alikasirika sana. Akaanza kumtafuta Linda. Alipofika kwa shangazi yake Linda, alimwona Linda akicheza na binamu zake.
Binamu zake walikuwa Tausi na Juma. Tausi alikuwa darasa la 4 na Juma alikuwa anasoma la 2. Baba yake alipomwona Linda, aliita, "Linda, mwanangu!" Linda alifurahi kumwona baba yake. Alimkimbilia kwa furaha.
Shangazi Linda alipomwona Baba Linda, alimwuliza, "Kwa nini ulimwacha Linda?" Baba Linda akasema, "Sikupenda kumuacha. Nilisafiri tu kikazi." Shangazi akasema, "Karibu tule." Baba Linda akasema, "Asante." Wakati wanakula, shangazi yake Linda alimuelezea kila kitu.
Shangazi akasema, "Lazima nimpeleke yule mama kituo cha polisi." Baba Linda alipotaka kumchukua Linda, Linda alimwambia kuwa alitaka kubaki na shangazi yake. Baba yake alikubali kumwacha. Baba Linda alimwahidi Linda kuwa atakuja kumtembelea mara kwa mara.

