

Ninaitwa Sania Muhammed. Nina kipaji cha uandishi wa mashairi ya kufunza. Mwalimu wa kiswahili amenisaidia kuendeleza kipaji changu kwa kunifundisha sifa za mashairi na jinsi ya kutunga na kughani. Ninafanya mazoezi ya sauti na utungaji.
Nina ndoto ya kuwaelimisha watu na jamii kwa kutumia kipaji changu. Nitaendelea kuwaza na kutunga mashairi yanayosisimua na yenye mafundisho. Pia nitatangaza kipaji changu kwa kujirusha mtandaoni ili watu wote wanione na wajifunze.
Mimi ninaitwa Josephina Ayubu. Kipaji changu ni kuimba. Nitaelimisha jamii kupitia nyimbo. Marafiki zangu wamenihamasisha kwa kusema nina sauti nyororo. Ninafanya mazoezi kabla ya kuimba. Nitaendelea kujifunza ili nikuze kipaji changu.
Aliyenisaidia kuendeleza kipaji changu ni mama yangu, ameniambia kuwa ili niwe muimbaji mzuri napaswa kufanya mazoezi ya kuimba sauti mbalimbali. Nikiwa mkubwa nitaelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira kupitia nyimbo.
Ninaitwa Khairati Hemedi. Nina kipaji cha kuimba. Nina sauti ya kuvutia na ninatarajia kuwa msanii mkubwa nikimaliza kusoma. Ninataka kukiendeleza kipaji changu ili hapo baadae nikitumie kuwaburudisha watu na kuwafanya wasiwe na huzuni.
Jina langu ni Zaituni Idd. Nina kipaji cha kuigiza. Kipaji changu kinanipa ujasiri wa kuzungumza mbele za watu. Nimekuwa naigiza mbele ya wanafunzi wenzangu nikiwaelimisha kuhusu umuhimu wa kusoma kwa bidii na kuwatii walimu na wazazi.
Ninaitwa Nairath Hassani. Nina kipaji cha kupika chakula kitamu. Ninajua kupika maharage, ugali na pilau. Nilipokuwa mdogo mama yangu alinifundisha ila kwa sasa ninaweza kupika vyakula vingi nyumbani. Nikiwa mkubwa nitakuwa mpishi hotelini.
Naitwa Safi George. Kipaji changu ni kuchora. Kipaji changu kinaweza kunipatia ajira na kuniongezea kipato. Dada yangu ndiye aliyenihamasisha kupenda kuchora na mpaka sasa najitahidi katika uchoraji.
Nimekuwa nikichora michoro mbalimbali kuonesha wanafunzi wakicheza rede, wakienda shuleni au kuelimishana kuhusu magonjwa vile vile waliovaa mavazi ya maadili na yasiyo na maadili.
Walimu wangu wamekuwa wakinisaidia bila kujua pindi waliponipatia kazi za kuchora darasani, hii imenisaidia kuweza kuchora. Nina ndoto ya kutumia kipaji changu kama kazi itakayonirahisishia maisha yangu nikiwa mkubwa.
Ninaitwa Nurath Nuhu. Kipaji changu ni kucheza mpira wa miguu. Mchezo huu ni muhimu kwani unaimarisha mwili. Aliyenihamasisha kucheza mpira wa miguu ni baba yangu. Nategemea kuwa mchezaji bora wa kimataifa na nimekuwa nikifanya mazoezi.
Aliyenisaidia kuendeleza kipaji changu ni mama yangu na amekuwa akinisisitiza mara kwa mara kufanya mazoezi ya viungo na kukimbia . Nina ndoto za kukikuza kipaji changu kwa kula vizuri na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.
Jina langu ni Jamila Said. Nina kipaji cha kucheza mpira wa wavu. Michezo hujenga na kuupa mwili nguvu. Dada yangu ananisisitiza kufanya mazoezi ya viungo . Nikiwa mkubwa nitaelimisha jamii kufanya mazoezi ili kulinda afya zao.
Mimi ni Asma Mohamedi nina kipaji cha kuimba. Nina sauti nzuri ya kuimba inayovutia watu. Ninajifunza kuimba kwa kufanya mazoezi kwa bidii ili sauti yangu iwe nyororo. Ninapenda nyimbo za kuburudisha, kuasa na kuhamasisha watoto wa kike.
Ninaitwa Farhiya Issa Madebe. Nina kipaji cha kucheza rede. Mchezo huu umesaidia kuwa mwepesi na kuweza kukimbia. Pia rede ya chupa inanisaidia kujua kuhesabu namba. Nikiwa nyumbani napenda kucheza rede na wadogo zangu Suhayra na Lulu.
Jina langu ni Asma Anzuruni. Nina kipaji cha kuimba. Ninaweza kuwaburudisha watu kupitia kipaji changu. Dada yangu ananihamasisha kukuza kipaji changu kwa kunionyesha wasanii wengine wanavyoimba. Ndoto yangu ni kuwa msanii mkubwa wa kuimba.
Ninaitwa Rujaina Mwalami. Nina kipaji cha uandishi. Ninaposhika kalamu na kuandika najisikia vizuri sana. Mama na walimu wangu wananisaidia kukuza kipaji changu. Nina ndoto ya kuboresha kipaji changu kwa kuandika vitu vya kuelimisha jamii.
Jina langu ni Sumaiya. Kipaji changu ni kuchora. Dada ananitia moyo na kuniambia nisikikatie tamaa kipaji changu. Ninataka kusoma zaidi ili niwe mwalimu wa uchoraji na niweze kuwasaidia wanafunzi wanaopata ugumu katika kujifunza uchoraji.
Ninaitwa Samia Bakari. Kipaji changu ni kuimba. Ninavutiwa na waimbaji ninaowaona kwenye televisheni na kuwasikia redioni. Nami nataka kuimba ili kuelimisha watu na kudumisha ushirikiano na upendo katika jamii yangu.
Naitwa Khayrat Munir. Mimi nina kipaji cha kuimba. Natumia muda wa ziada kufanya mazoezi ili niweze kuimba vizuri. Kila ninapoimba mwili wangu huchangamka sana. Nikiwa mkubwa nitaimba ili kuwaburudisha watu wengine.
Jina langu ni Ashura Al-haji. Nina kipaji cha kuimba. Ninakuza kipaji changu kwa kufanya mazoezi ya kuimba nyimbo mbalimbali. Nina ndoto ya kuwa muimbaji bora na kuifanya jamii yangu ipende muziki. Nitapata fedha nyingi nikiimba muziki.
Jina langu ni Amina Omary. Kipaji changu ni kucheza mchezo wa rede. Hakuna mtu yeyote anayeweza kunishinda kwenye mchezo huu. Mchezo wa rede ni muhimu kwani unanifanya naimarisha viungo vyangu vya mwili kama vile miguu, mikono na shingo.
Mimi ninaitwa Rukia Ramadhani. Nina kipaji cha kuchora. Ninafanya mazoezi ya kuchora kila nikipata muda, shuleni au nyumbani.Marafiki zangu waliniomba nichore picha nami nikachora picha nzuri ya samaki. Nitawafundisha na wao wajue kuchora.
Jina langu ni Neema Michael. Kipaji changu ni kuruka kamba. Wazazi wangu wamenitia moyo kuendeleza kipaji changu. Naamini hata yakitokea mashindano ya michezo mimi ndio nitashika namba moja kwenye kuruka kamba katika shule yetu.
Ninaitwa Mwanamosi Yahya. Nina kipaji cha kuimba.Mimi hupenda kusikiliza nyimbo mbalimbali za bongo fleva hasa nikiwa natembea barabarani ninaporuhusiwa kutoka shuleni kwenda nyumbani. Nina ndoto ya kuwa msanii mkubwa wa kuimba hapo baadae.
Jina langu ni Aisha Ramadhani. Mimi kipaji changu ni uchoraji. Ninapenda sana kuchora. Mwalimu akitupa kazi ya kuchora darasani huwa nafurahia sana kwani naweza kufanya mazoezi ya kuchora na pia kuwafundisha wanafunzi wengine darasani.
Jina langu ni Paskalia Inyasi. Kipaji changu ni kucheza muziki. Kucheza kunasaidia mwili wangu kuwa mwepesi na mkakamavu. Mimi na dada yangu hufanya mazoezi ya kucheza kila siku jioni tukimaliza kuwasaidia wazazi kazi za nyumbani.
Jina langu ni Yusra Mohamedi. Nina kipaji cha kuimba. Natamani kukifanya kipaji changu kiwe bora zaidi kwa kufanya mazoezi. Ndoto zangu ni kuwa msanii mkubwa nipate hela nyingi ili niweze kutoa misaada kwa watoto yatima na watu wasiojiweza.
Mimi naitwa Rujayna Rashid. Nina kipaji cha kusuka nywele. Ninajua kusuka mitindo ya minyoosho,ndizi, karoti na kilimanjaro.Bado najifunza kusuka rasta.Nimefundishwa kusuka na mama yangu. Nina ndoto ya kufungua saluni ili nisuke watu wengi.

