

Sisi ni wasichana wa darasa la 5 na la 6 kutoka Shule ya Msingi ya Mwasi Kaskazini. Tumeandaa kitabu hiki katika klabu yetu ya Hadithi Zetu mwaka wa 2025.
Tunatumaini ndoto zetu zitawatia moyo watu wengine kuwa na ndoto kubwa maishani na kwenye jamii zao.
Ninaitwa Tunu. Ninataka kuwa mwalimu. Nitawaelimisha wanafunzi kujiwekea ndoto zao. Ninataka kufanya kazi ya ualimu ili niwape watoto maarifa mema. Ninataka kuwapa watoto vitabu vya kujisomea, wasome kwa umoja na ushirikiano. Ninataka wasome vitabu nyumbani sio shuleni tu.
Pia wafurahie kusoma na watu wengine. Nataka kuhakikisha wanafunzi wote waende shule. Watoto wasikae nyumbani.
Nataka kuishi Dar es Salaam ili nikae karibu na wazazi wangu. Ninataka kuongea lugha za Kiswahili, Kiingereza, na Kiha. Nataka kuongea Kiha ili kudumisha lugha zetu.
Ninaitwa Happiness. Nina ndoto ya kuwa daktari ili niwasaidie wagonjwa na kupunguza vifo. Ndoto yangu imetokana na nilivyoumia kifo cha mdogo wangu kwa kukosa matibabu na kufariki. Mimi napenda kuwa daktari ili kuwasaidia wagonjwa wasipoteze maisha.
Nitawapa wagonjwa dawa na kuwachoma sindano
ili wapone. Watu wenye magonjwa yasiyo na dawa kama ukimwi nitawapa ushauri wa vyakula vya kula na kutokula, na wasifanye kazi ngumu, wafanye kazi nyepesi kama kuosha vyombo na kudeki.
Nina ndoto ya kuleta mabadiliko makubwa katika jamii kwa kuondoa umasikini na kusaidia walemavu wasiojiweza.
Pia nitawasaidia walevi na kuwapa ushauri wanywe kiasi.
Ninataka kuishi Arusha ili niwe karibu na wazazi wangu. Mungu akinisaidia sitaishi Tanzania tu, pia nitaishi nchi za nje kama China. Nitaongea Kiingereza, Kiswahili na Kichina. Kimbulu nitajifunza nitakapoenda Karatu kwa bibi yangu.
Ninaitwa Helena. Nataka kuwa mwasibu wa benki. Nitamfanya bosi wangu ajivunie kuwa na mfanyakazi kama mimi. Ndoto yangu ilitokana na kwenda benki na bibi. Bibi alinieleza mwasibu anafanya kazi gani. Ndipo nilipoanza kupenda hiyo ndoto.
Nataka nifungue duka la nyumbani. Nitauza
bidhaa za kila aina. Nitaweka duka la mpesa na bidhaa tofautitofauti ili watu waweze kupata huduma kwa karibu. Nataka kuwa na familia yenye maadili inayozingatia heshima na isiyovunja tamaduni.
Nina ndoto ya kuelimisha wanawake na wanaume kwamba bora kuajiriwa au kujiajiri. Usipende
kukaa nyumbani bila shughuli yoyote ili uweze kusomesha na kulisha watoto wako, waende shule.
Nataka watu wawe wachapakazi na wasikate tamaa maishani. Washirikiane na wasitengane wala kubaguana. Waishi kwa upendo na furaha, wapate kazi nzuri, na kila mmoja atunze familia yake.
Ninaitwa Eliza. Ndoto yangu ni kuwa rubani. Nitarusha ndege vizuri na watu kufurahia. Ndoto yangu itanisaidia kujua watu nisiowafahamu na kuwasaidia watu wanaoenda nchi za nje na wanaorudi Tanzania. Mimi nilipenda kazi hiyo tangu nilipokuwa mdogo.
Ninataka niwe naongea Kiswahili, Kiingereza, na Kichaga. Nitaomba nifundishwe lugha nyingine na makabila tofautitofauti. Ninapenda kufundishwa lugha kama Kimbulu, Kimaasai, Kinyakyusa, Kikorea, na Kifaransa ili niweze kujua makabila tofauti ya kupendeza.
Ninataka kuwa na familia ya watoto 3 watakaonisaidia maishani na jamii kwa ujumla. Nitawafundisha kusoma, kuandika, na kuhesabu.
Ninapenda wanajamii wangu kwa sababu wananikosoa wakati sielewi cha kufanya au wanapoona kitu fulani hakiko sawa. Pia wananifundisha tabia njema.
Ninaitwa Judith. Ndoto zangu ni kuwa mwalimu ili kuwasaidia wanafunzi waweze kusoma, kuandika, na kuhesabu. Nitafundisha wanafunzi umoja, upendo, ushirikiano, na mshikamano katika jamii na michezo mbalimbali kama mpira, rede, kuruka kamba, kucheza netball, kukimbia, na mdako.
Ninapenda watoto wasome kwa bidii. Nitahakikisha wote wanakuja shuleni. Pia ninapenda waje na nidhamu, wawe na utii, na wawe wakisalimia watu wazima na hata wadogo.
Ninataka kuishi Dar es Salaam kwa sababu mamangu anakaa huko.
Ninataka kusoma mpaka
chuo kikuu. Ninaomba mungu anisaidie kufaulu Form 5 na 6 ili niweze kufikia ndoto zangu.
Ninataka kuongea lugha za Kiingereza na Kiswahili fasaha.
Ninapenda nchi iwe na upendo, isiwe na magombano, iwe na amani na furaha.
Konjiisuo? Umenipata?
Mimi ni Sofia. Nina ndoto ya kuwa daktari wa kutibu watu. Nimependa hiyo kazi kwa sababu ninaona katika jamii watu wanakufa sana na kupata magonjwa mengi. Nataka kuwa daktari wa kutibu watu wote ili wasije wakafa na kuwasaidia watu wote. Nitatibu watu kwa ustadi mkubwa sana.
Ninataka kusoma mpaka chuo kikuu na kumaliza shahada ya udaktari.
Pia ninapenda kulima. Nilifundishwa na bibi. Nyumbani ninafuga na nina bustani ya maua na mboga.
Ninataka kuishi mimi na wazazi wangu kwenye nyumba moja.
Nitakuwa ninaongea Kiswahili,
Kichaga, Kiingereza, na Kimaasai. Nitajifunza lugha nyingi. Nitaongea Kiingereza kazini na Kichaga nikiwa kijijini.
Nitawasaidia wazazi na walezi. Nitawasaidia walemavu, watoto yatima, na watu masikini. Kutoa ni moyo si utajiri. Ninapenda kuwasaidia watu wote, wadogo kwa wakubwa, maadui na marafiki.
Ninaitwa Deborah. Ndoto yangu ni kuwa fundi wa kushona nguo mbalimbali wa kila dizaini. Nilimwona dada yangu akiwa anashona nguo. Nilikuwa nashona nguo na sindano ndogo nikiwa darasa la tano na kujifunza kushona nguo ndogondogo. Nikiwa mkubwa nitaendelea na ndoto yangu ya kushona nguo.
Pia, nina ndoto ya kuotesha mbogamboga na kuuza ili nipate hela na kujinunulia vitu vidogovidogo, kwa mfano kalamu na penseli. Nitaotesha na kuuza na kupata fedha na kuwapa wazazi wangu. Ninataka kusoma mpaka chuo kikuu. Ninataka kuongea Kiswahili na Kichaga.
Ninaitwa Onesma. Ndoto yangu ni kuuza duka kubwa baadaye. Duka langu litakuwa la kifahari na watu watavutiwa na duka langu. Nataka mpaka nchi za nje zijue kuwa nina duka la kila kitu. Nitatimiza ndoto yangu kwa kuifanyia mazoezi ya kuuza vitu vidogovidogo kama nyanya, karoti, na ngogwe.
Nina ndoto ya kuwajalia baba na mama yangu na kuwajengea nyumba na kuweka geti na mlinzi.
Ninataka kuishi Mwanza. Nitanunua kiwanja kwa ajili ya duka na nyumba yangu.
Nitakuwa ninaongea Kiswahili, Kiingereza na Kichaga. Mtu akija dukani kwangu akiongea Kichaga nami naongea Kichaga.
Mimi ni Juliet. Ndoto yangu ni kuwa mwalimu. Nitawafundisha wanafunzi kusoma na kuandika, afya, na mazingira. Nataka kufanya shughuli ya ualimu ili kuleta mabadiliko katika jamii. Kama wamekosea nawarekebisha. Kama kuna tatizo nawasaidia. Ninataka kuishi Dar es Salaam kwa sababu
kuna hewa nzuri, hakuna fujo, pia panavutia kabisa. Ninataka kusoma mpaka chuo kikuu ili nitimize ndoto zangu. Ninataka kuongea lugha mbalimbali mfano Kiswahili, Kiingereza, na Kichaga.
Nataka kuwa na familia yenye furaha na amani bila kugombana, matusi, na kusengenyana.
Sisi tunapenda jamii yenye upendo, mshikamano, amani, na nidhamu kwa wakubwa na kwa wadogo. Tuna ndoto ya kuwa na jamii yenye kusalimiana ili kuheshimiana na kupendana. Tunataka wanajamii washirikiane kwenye misiba, sherehe, na hitima.
Tuna ndoto ya kuwa na jamii yenye michezo kwa sababu ya kuimarisha ushirikiano katika jamii. Michezo husaidia kuchangamsha viungo vya mwili na kufurahisha mwili, na kufahamu watu usiowafahamu. Tuna ndoto ya kuwa na jamii yenye uwanja wa kuchezea, magoli, mipira, na jezi.

