

Sisi ni wasichana wa darasa la 5 na la 6 kutoka Shule ya Msingi ya Mwasi Kaskazini, mkoani Kilimanjaro. Tumeandaa kitabu hiki katika klabu yetu ya Hadithi Zetu mwaka 2025.
Tunaamini kwamba msichana ni mtu wa kipekee. Soma kitabu hiki ujifunze umuhimu wetu sisi wasichana kwenye jamii!
Ninaitwa Winifrida. Msichana ni mvumilivu. Anaweza kufanyiwa jambo lolote la kunyanyasika na akavumilia.
Msichana ni mwenye upendo. Watu wengine humbagua msichana wakisema hana haki katika jamii. Lakini msichana anaweza kumsaidia mlemavu na mtu yeyote mwenye shida.
Si mbaguzi kwamba huyu ni rafiki na huyu ni adui. Msichana anajali wengine. Unaweza kukuta msichana ameumia lakini anamjali mtu mwingine aliyeumia.
Watu huwachukulia wasichana kama si watu wa kusoma, ni watu wa kufanya kazi za nyumbani. Lakini watu
wanaomdharau msichana baadaye hujuta kwa sababu angeweza kusoma hadi chuo kikuu na kusaidia familia.
Dunia inatakiwa kujua msichana ana haki kama mvulana, na hatakiwi kubaguliwa. Waishi naye kwa upendo na furaha na asiolewe bali apelekwe shule akasome.
Ninaitwa Catherine. Dunia inajua msichana ni mwenye nguvu, ni hodari, na ana akili. Anasali rozari.
Kaka kazi yake ni kucheza tu akijua kazi zote msichana anafanya, kwa mfano kufua nguo nyingi, kudeki, kuosha vyombo, kufagia, kuteka maji, kubeba vitu vizito, kupika,
kufuga kuku, na huku kaka amekaa tu akicheza zake. Wala hana habari, yeye yuko zake tu huku dada akiteseka.
Watoto wa kike wakifika Form 4 wanaozeshwa ili kupata fedha. Mvulana anaitwa jembe langu huku wasichana wakiitwa wapumbavu. Hawajui msichana ni mwenye haki.
Ninaitwa Loveness. Jamii ithamini wasichana kwa sababu ni wachapakazi. Wanaweza kufanya kazi kama kulima, kufua, kudeki, kufuga, biashara ndogondogo, kwenda sokoni, kuzaa watoto, kulea watoto, na kumnyonyesha mtoto.
Watu wanawachukulia wasichana hawana faida kwa sababu
wanasema ukisomesha msichana anayefaidika ni mume wake. Lakini wengine wanaona wasichana ni wenye faida nyingi kwa sababu wanashirikiana na wenzao katika shida na raha, mfano msiba, sherehe, harusi, na hitima. Hawaachi wenzao kuteseka. Watahuzunika na wewe,
watasherehekea na wewe.
Wasichana huwasaidia walemavu, wazee, watoto, wagonjwa na wanawake waliojifungua. Mzee akimtuma dukani, ataenda. Wanawake waliojifungua hawataweza kufanya kazi, hivyo msichana atamsaidia. Maana msichana ni mwenye upendo mkubwa.
Mimi ninaitwa Joselini. Najivunia kuwa msichana kwa sababu nitasaidia jamii baadaye katika shida.
Msichana ni mwenye nguvu. Anafanya kazi nzito, kwa mfano kuchota maji, kubeba mtoto, kumsaidia mama kupika, kumsaidia mama shughuli mbalimbali nyinginezo.
Msichana ni mtu mwenye kusaidia katika shida na raha. Mfano, mwenzake akiwa hana kalamu, anaweza ampe au akiwa amepoteza humsaidia kutafuta au kumwombea kwa mwenzake.
Msichana ni mwenye upendo, mfano mwenzake akiwa amefiwa humpa ushauri. Msichana ni
mwenye kufikia malengo yake. Mfano, kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zake.
Watu wanawachukulia wasichana ni watumwa, na wengine wanawachukulia ni wenye kuwasaidia katika maisha yao. Watu wengi wanawafanyisha kazi.
Kwa mfano, wanawatuma tu, wanawabebesha mizigo mikubwa, na wanawabebesha watoto hadi wanakosa muda wa kujisomea, kujifunza, na kutimiza ndoto zao.
Mimi nataka dunia ijue kwamba wasichana wa Mwasi ni wenye nguvu. Mfano, wanaweza kubeba mizigo mizito,
kuchota maji, kufagia, kufua nguo, kudeki, na kupika. Msichana ni mtu mwenye kujiamini, mfano anaweza kusimama mbele ya watu na kuwapa ushauri kuhusu mambo mbalimbali.
Najivunia kuwa msichana kwa sababu najijali na nawajali wenzangu katika shida na raha.
Ninaitwa Florensiana. Wasichana ni wachapakazi. Wazazi wanatutegemea nyumbani na tunasaidia walimu shuleni.
Zamani wasichana walikuwa hawapelekwi shule. Ni wavulana ndio walikuwa wanapelekwa shule. Wavulana wakirudi shuleni wanataka chakula.
Najivunia kuwa msichana kwa sababu nina utu. Ninawasaidia watu mbalimbali kama wazazi na wazee. Tunatakiwa tupewe elimu. Wazazi wanataka kutuozesha mapema ili wapate mahari.
Nataka dunia ituchukulie kuwa wasichana ni wachapakazi, na watu wenye ushirikiano.
Ninaitwa Jesca. Msichana ni mchapakazi. Watu wengine wanamtegemea. Msichana ni shujaa, lakini hapewi haki kama mvulana. Wasichana wengine wananyimwa haki ya kusoma siku moja moja ili wafanye kazi kama kulisha ng'ombe, kupika, kuosha vyombo, kuchota maji, na kufua.
Ninaitwa Angel. Msichana ni mtu anayejitolea kufanya kazi mbalimbali kama kufua, kudeki, kuosha vyombo, kuchota maji, kufagia, kulima, kupika, n.k. Msichana ni mtu mwenye nguvu, utu, huruma, na upendo.
Msichana anaweza kusimama mbele ya maelfu ya watu.
Watu wanawachukulia wasichana katika jamii ya Mwasi kuwa ni wafanyakazi na wala siyo wenye haki ya kupata elimu. Lakini wasichana wana haki ya kupata elimu kwa sababu tuna bidii katika masomo.
Watu wajue wasichana ni wenye haki ya kupata elimu kama wavulana.

