

Unajua lugha zipi? Unazitumia wapi, ukiwa na nani, na kwa malengo gani? Unatarajia kutumia lugha zipi mbeleni?
Wanafunzi wa Maktaba ya Jamii Cheche walichunguza maswali haya kwa kina. Walichora ramani kuonesha matumizi ya lugha mbalimbali katika maisha yao, wakitumia rangi tofauti kuwakilisha lugha tofauti. Waliandika, kujadiliana, na kufundishana lugha zao. Matokeo ni kitabu hiki, pamoja na 'Tunajua Lugha Nyingi!', vinavyoonesha uwezo wao mpana wa lugha mbalimbali.
Mimi ninaitwa Idris. Ninajua lugha ya Kichaga. SHIMBONI inatumika kusalimiana kwa jamii za Wachaga. Nimejifunza Kichaga kwa bibi huku Monduli. Lugha za Wachaga zina umuhimu mbalimbali mfano salamu na kuongea na mtu mwenzake kwa lugha ya Kichaga.
Lugha nyingine ni Kiarabu. السلام عليكم ni lugha ya Kiarabu inayotumika kusalimiana na jamii za Kiarabu.
Mfano mwingine wa lugha ya Kiarabu ni بسم الله. Lugha hiyo ni mwanzo wa kurani ambayo huandikwa mwanzo wa kitabu cha kurani kabla ya kusoma kurani. Nimejifunza Kiarabu kwa babangu na pia msikitini.
Lugha nyingine ni Kipare. Waendelea zeze ni lugha ya Kipare inayotumika kusalimiana na Wapare wenzake na kumtakia mtu habari nzuri.
Nimejifunza Kipare kwa baba mkubwa anayeishi Arusha.
Vinywaji vya Wachaga ni mbege, vinywaji vya Waarabu ni soda, na vinywaji vya Wapare ni soda.
Mimi ninatoka katika tamaduni za Kichaga na Kiarabu na ninajivunia katika tamaduni zangu kwa sababu tamaduni za Kichaga ni wakarimu na ni wasikivu.
Mimi ninaitwa Anita. Katika darasa la Maktaba ya Cheche nimejifunza lugha zifuatazo ambazo ni Kimaasai na Kiswahili. Ninatumia lugha za Kimaasai na Kiswahili nikiwa kijijini kwetu na nikiwa nasafiri. Nyumbani natumia Kiswahili. Lugha hii inanisaidia kuishi katika mazingira mbalimbali.
English: My name is Anita. My father's name is Elijah. My mother's name is Rebecca.
Kimaasai ninatumia nikiwa nyumbani. Kiingereza ninakitumia nikiwa shuleni kwenye kujibu maswali. Kiswahili nakitumia katika mazingira ya nyumbani na shuleni na mtaani. Ninajua kuhesabu kwa Kiingereza, kwa mfano one, two, three, four, five. Kimaasai nimejifunza nikiwa kijijini kwa sababu mimi nimezaliwa huko.
Ninatumia lugha ya Kiswahili nikiwa na marafiki zangu. Nimejifunza kwa kusikiliza watu wanavyoongea na kwa kusoma vitabu mbalimbali.
Ninataka kujua lugha zifuatazo, kwa mfano Kichina, Kifaransa, Kijapani, na Kiingereza zaidi. Ninataka kutumia lugha hizi nikiwa katika nchi mbalimbali.
Mimi ninaitwa Josefu. Ninajua lugha mbalimbali. Lugha ya kwanza ni Kijaluo. Omera ni mvulana. Na lugha nyingine ni English, ni kama vile grandmother ni bibi na grandfather ni babu. Ninajua lugha nyingine ni Kiswahili, ni lugha inayojulikana hapa Tanzania. Lugha ya Kijaluo nilijua nikiwa kwa bibi yangu huko Mwanza, pia nilijifunza lugha mbalimbali kama Kisukuma. Lugha nyingine ni Kimaasai. Bibi ni kokoo.
Nikiwa mkubwa nitajua lugha mbalimbali. Nimejifunza kuhusu jamii za kale. Hapo mwanzo, nilijifunza kuhusu lugha ya Kisambaa maana baba ni Msambaa, ila sikumbuki lugha hata moja ila nitajua. Kipare sikumbuki hata moja.
Kijaluo nilijifunza nikiwa Mwanza na Kisambaa nilijifunza nikiwa Tanga.
Lugha ya mwisho ni Kiingereza. Nilijifunza nikiwa Arusha. Nimejifunza nikiwa ninasoma shuleni. Lugha nyingine zina umuhimu wa kukutambulisha katika nchi mbalimbali. Unapoenda unakuta wanaongea Kisukuma ila sikumbuki hata moja ila nitakuja kujifunza nikiwa mkubwa.
Kabla sijafikisha umri wa miaka kumi na tatu nitajifundisha lugha mbalimbali kama Kifaransa na Kichina.
Mimi ninaitwa Frida. Ninapenda Kiingereza. Nimefundishwa na wazazi wangu kuongea Kiingereza na Kiswahili nikiwa na familia yangu. Nikiwa na rafiki yangu naongea naye Kiswahili. Familia yangu inanisaidia kujua Kiingereza. Pia nimejifunza kutoka shuleni. Kwa mfano, My mother is holding the door. Baby is holding a ball.
Ninataka kujua Kiingereza kwa sababu dada yangu amenifundisha. Ninapenda kuongea lugha ya
Kiingereza nikiwa kwa dada yangu na nikiwa na familia yangu. Ninapenda kujifunza Kiingereza. Dadangu ananifundisha sana.
Nimejifunza Kichaga: mro, mawoko, marende.
Ninapenda kuongea Kiingereza na watu wengine na kuwafundisha wenzangu Kiingereza. Ninapenda wenzangu wajue Kiingereza kwa sababu Kiingereza kinanisaidia kwenye maisha yangu ya baadaye. Kwa mfano, nikiwa mkubwa nitawafundisha watoto wangu Kiingereza.
Ninaitwa Emmanuel. Najua lugha mbalimbali ambazo ni Kimaasai, Kifaransa, na Kimeru. Natumia lugha ya Kimaasai nyumbani, nikikutana na mtu njiani anayejua Kimaasai, na marafiki zangu. Mwanzoni nilikuwa natumia kwa bibi yangu. Na sasa nakijua sana Kimaasai na nakitumia nikiwa naongea na mjomba wangu, bibi yangu, ndugu zangu, na mama yangu. Ninatumia Kiswahili nikiwa shuleni na saa nyingine nikiwa nyumbani.
Nilijifunza Kiingereza shuleni. My name is Emmanuel. My father's name is Laizer. My mother's name is Paulina.
Lugha hizi zina umuhimu wa kusaidia jamii na zinanisaidia kuongea na wageni mbalimbali na watu mbalimbali nchini. Lugha hiyo ya Kimaasai nimejifunza kwa bibi yangu na hizo zingine ni ndoto yangu. Lugha ya Kimeru najua kidogo kwa sababu babu yangu ni Mmeru na aliwahi
kumfundisha mama yangu na mama yangu alinifundisha. Na pia baba yangu ni Mmeru.
Mbeleni nataka kujua lugha ya Kifaransa kwa sababu ndoto yangu imependa lugha hiyo. Dada yangu alikuwa anataka kwenda Ufaransa kupata ajira huko, lakini haikutokea.
Nategemea kuongea lugha ya Kifaransa kwenye nchi mbalimbali au nikiwa na wageni na nikiwa nafanya kazi yangu au kwenda kutembelea.
My name is Aziel. Leo ninaelezea lugha ninazozijua. Mimi ninajua lugha za Kigogo, Kiingereza, na Kikaguru. Nimetumia Kigogo na Kiswahili nikiwa kijijini kwa wazazi wangu huko Dodoma. Lakini nikiwa Kongwa kwa shangazi yangu, ninatumia lugha za Kiswahili, Kigogo, na Kikaguru pia.
Salamu kwa Kigogo ni solowenu, kwa Kikaguru ni bamsindile. Kwa Kiingereza salamu ni how are you!
Hizi lugha zina umuhimu sana kwangu kwa sababu ninazipenda kuongea nikiwa na rafiki zangu. Pia nimejifunza Kimaasai. Salamu ni takwenya.
Lugha za Kigogo na Kiswahili nimefundishwa na wazazi wangu na shangazi yangu. Na Kikaguru nimefundishwa na shangazi yangu na rafiki yangu ambaye ni Mkaguru.
Nikiwa nyumbani, tunaongea Kigogo na Kiswahili. Sokoni, ninatumia Kiswahili, Kigogo, na Kiingereza. Kwenye michezo, tunakutana na watu wenye lugha mbalimbali lakini tunatumia lugha ya Kitanzania ambayo ni Kiswahili ili kuelewana kwa urahisi.
Na nitawafundisha ambao hawazijui ili wazijue na niweze kuongea nao pia.
Mimi ninaitwa Mery. Ninajua Kimaasai, Kiswahili, Kichaga, na Kiingereza. Ninatumia Kimaasai na Kiswahili nikiwa na rafiki yangu. Nikiwa na dada yangu ninatumia Kimaasai, Kiswahili, na Kiingereza. Kiswahili ninatumia nikiwa sehemu mbalimbali, kwa mfano nikiwa nyumbani, kanisani, nikiwa napika na kufua nguo. Kina umuhimu katika
maisha ya jamii yetu, kinanisaidia kujijua na kujitambua. Nikisikia mtu anaongea nami nakariri hapo hapo elukunya inkejek enkoshoke enkonyek.
Kimaasai ninajifunza kutoka kwa mama. Kiingereza najifunza shuleni. Kichaga najifunza Maktaba ya Cheche.
Ninataka kujifunza Kijapani, Kichina, na Kikorea ili nijue
lugha mbalimbali. Kimaasai natumia nikiwa na mama yangu nyumbani na nikiwa na rafiki yangu shuleni. Kichaga nimejifunza Maktaba ya Cheche. Kiingereza nimejifunza shuleni na nyumbani kidogo. Ninapenda kujua lugha ya Kiingereza. Sijui Kichina, Kifaransa, Kikorea, Kijapani, na Kihispania. Ninataka kujua lugha hizo.
Mimi ninaitwa Wiliamu. Ninajua lugha za Kiingereza, Kiswahili, na Kikuria. Kwa mfano, ukitaka kusalimia kwa Kikuria unasema tata sokoro mwita. Ukitaka kusalimia kwa Kiingereza unasema Good morning. Pia ukitaka kusalimia kwa Kiswahili unasema Shikamoo.
Lugha ya Kikuria ni lugha ya familia. Ninataka kujua lugha ya Kikuria. Nilijifunza katika familia yetu.
Lugha ya Kiswahili nilijifunza nilipozaliwa. Lugha ya Kiingereza nilijifunza shuleni na pia nikiwa na marafiki. Nilijifunza kwa kuwaiga watu, hasa baada ya kuhamia Kenya. Kiingereza kina umuhimu kwenye maisha yangu ya baadaye.
Nikiwa mkubwa, ninataka kufanya kazi ya utalii au engineer. Nikifanya kazi zangu, nikitaka kuongea na wazungu, nitatumia Kiingereza.
Kwa mfano, nikipeleka watalii Kilimanjaro, nitakuwa naongea nao kwa Kiingereza.
Lugha ya Kikuria nitatumia wakati nimeenda kuwasalimia watu wa familia. Nikienda Kenya kuwatembelea ndugu zangu, nitatumia Kikuria kuwasalimia na kuongea nao na kuwauliza Kenya panaendeleaje siku hizi huko.
Ninaitwa Musa. Napenda lugha ya Kiingereza kwa sababu lugha hii inatumika shuleni mara nyingi kuliko Kiswahili. Pia Kiswahili na Kimaasai ninatumia nyumbani. Kwa Kimaasai, nyumba inaitwa engaji. Kwa Kiingereza, kusalimia unasema Good morning. Lugha ya Kimaasai ina umuhimu kwenye maisha yangu kwa mfano kunisaidia nikiwa nauza dukani. Nimejifunza lugha hii ya Kimaasai kutoka kwa watu mbalimbali Umaasaini.
Mbeleni nataka kujua lugha za Kifaransa, Kichina, na Kichaga. Nataka kutumia lugha hizi nikifanya kazi zangu za utalii. Nitaomba nifundishwe na watu wanaojua lugha hizo.
Napenda kujifunza lugha ya Kiingereza kwa sababu shule unalazimishwa kuongea lugha ya Kiingereza mpaka unavalishwa bango ukiongea Kiswahili.
Bango hilo limeandikwa Speak English maana yake ongea Kiingereza. Ukivalishwa unajisikia vibaya maana wenzako wakikuona watakucheka. Hapo unatakiwa kumtafuta mtu mwingine ambaye anaongea Kiswahili ndio umpe mtu huyo na yeye atafute mtu mwingine anayeongea Kiswahili. Pia inatupa changamoto kwa sisi wanafunzi haswa wa kidato cha kwanza, wengine hawajui Kiingereza wanaishi Umaasaini.

