Mtoto pori
Billy Artist
Wiehan de Jager

Mango ni mtoto wa miaka mitano asiyejua kuongea. Aliishi na wazazi wake katika kijiji cha Mkongo kilichopakana na mapori makubwa.

Wazazi wake ni wakulima na wafugaji pia. Waliuza mazao na wanyama waliofuga kujipatia pesa.

1

Wazazi wake walifanya kazi kwa bidii sana. Hali hii iliwapelekea kutokuwa makini na mtoto wao.

Siku moja Mango alipokuwa akicheza, aliwaona ndege wazuri mno. Bila kusita, aliamua kuwafuata mpaka akatokomea porini.

2

Wanakijiji walipopata habari hiyo waliungana na wazazi wake ili kumtafuta Mango. Walizunguka porini bila mafanikio.

Kwa upande wake, Mango alikuwa amepata marafiki wapya wakiwemo wale ndege na Nyani. Alicheza nao bila shida yoyote.

3

Maisha yake ya porini hayakuwa ya shida. Alikula matunda na mimea mwitu aliyoletewa na marafiki wake wapya.

Katika marafiki wote, Nyani alikuwa mtundu na hodari wa kukwea miti. Alimfundisha Mango ili kujilinda na wanyama wakali, pia alimkutanisha na Twiga.

4

Nyani hakukomea hapo, alimtembeza Mango safari ndefu mpaka kwa Kobe, mfalme wa upole porini. Mfalme huyu alikuwa mtulivu sana asiyependa vita.

Kobe alimpenda Mango na kuamua kuwa naye muda mwingi kumzidi Nyani.

5

Jambo lile halikumpendeza Nyani hata kidogo. Nyani alimkataza Mango asiendelee kuwa na Kobe muda mwingi. Alidai kwamba Kobe ni mpole hangeweza kumtetea Mango mbele ya wanyama wakali.

Mango hakusikia ushauri wa Nyani, aliendelea kumfuata Kobe.

6

Kobe alipenda kumbeba Mango mgongoni mwake na kumtembeza sehemu mbali mbali. Hakujali kuwa kuna wanyama wakorofi wasiopenda watu.

Siku moja, walifika katika mapango la Nyoka. Nyoka alijificha mapangoni akihofia adui zake.

7

Nyoka ni mkorofi sana. Baada ya kuona kuwa binadamu amemfuata hadi pangoni, alimtoa Mango mgongoni kwa Kobe na kutokomea naye pangoni.

Alimpa Mango masharti ya kumuimbia mpaka apate usingizi la sivyo angemmeza. Mango aliimba!

8

Nyani na Twiga waliposikia habari za Mango kukamatwa na Nyoka, waliamua kwenda kumuokoa.

Walimchukuwa Mango na kumrudisha nyumbani kwao. Wazazi wake walifurahi sana, wakawapa zawadi ya chakula na matunda kwa wema wao.

9
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Mtoto pori
Author - Billy Artist
Illustration - Wiehan de Jager
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs