

Rafiki zake Amani walikuwa na wanyama, wadudu, ndege au samaki vipenzi.
Amani alitamani sana kuwa pia na mnyama kipenzi.
Aliamua kuwatembelea babu na nyanya yake ili wamshauri katika maamuzi yake.
Babu alimuonyesha picha za ndege tofauti na kumweleza ubora wao. Amani alitega masikio na kusikiliza.
Huyu ni kasuku. Ana rangi nyingi maridadi na unaweza kumfunza kuongea.
Chakula chake ni wadudu na nafaka na anahitaji nyumba ndogo sana. Unaweza kuiweka nyumba yake sebuleni.
Huyu ni jogoo. Ana rangi nyingi maridadi na anatufaa kwa nyama.
Anaweza kukuamsha asubuhi na mapema. Huwika alfajiri. Hula wadudu, majani na nafaka.
Huyu ni mbuni. Ni ndege mkubwa kuliko wote na chakula chake ni nafaka.
Anatufaa kwa nyama, ngozi na manyoya. Ukimfuga atahitaji chakula kingi, nyumba kubwa na uwanja mkubwa.
Huyu ni heroe. Chakula chake ni wadudu na samaki.
Ana rangi maridadi ya waridi na anapenda maji.
Anatufaa kwa utalii. Huwezi kumfuga bila kibali maalumu.
Huyu ni njiwa. Chakula chake ni nafaka, wadudu na majani.
Anatufaa kwa nyama. Ni ndege mpole na anahitaji nyumba ndogo tu. Ni rahisi kumtunza.
Huyu ni bata-maji. Ana rangi nyeupe maridadi.
Anapenda kuishi karibu na maji.
Ni mkali na anaweza kuwatisha watu. Ukimfuga utahitaji kidimbwi cha maji.
Huyu ni kunguru. Ana rangi nyeusi na chakula chake ni wadudu na matunda.
Utahitaji kibali maalumu kumfuga.
Huyu ni kanga. Ana madoadoa ya kupendeza.
Chakula chake ni wadudu, nafaka na majani.
Ana nyama tamu sana na anatufaa pia kwa mayai.
Huishi nje na anahitaji nyumba ndogo tu.
Huyu ni bundi. Chakula chake ni panya na wanyama wengine wadogo.
Anapenda kufanya kazi yake usiku na ana macho makubwa ya kuona mbali. Waafrika wengi huamini huleta bahati mbaya.
Huyu ni tausi na ana rangi nyingi maridadi. Anajulikana kwa maringo yake.
Chakula chake ni nafaka na wadudu. Utahitaji nyumba kubwa na uwanja kumfuga.
Huyu ni kuku. Chakula chake ni nafaka. Hutufaa kwa mayai na nyama. Ni mpole na mahitaji yake ni maji, majani na nafaka.
Anahitaji nyumba ndogo na uwanja wa kuchakura.
Baada ya babu kumweleza ndege tofauti, Amani alisema, "Asante sana babu. Nitamchagua kuku, nitamlisha nafaka, naye atanipa mayai."
"Uamuzi mwema," babu akampongeza.

