

Hapo zamani za kale paliishi Ng'ombe, Ndama na Fisi. Walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Fisi alikuwa akila nyasi pia, ingawa haikumpa ladha wala shibe.
Kila wakati walienda malishoni pamoja. Mara kwa mara Fisi alishikwa na tamaa ya kula nyama.
Fisi alipokuwa akigeuka kumtazama Ndama, alianguka kwa shimo lililokuwa karibu. Ng'ombe alidondokwa na machozi kuona hivyo.
"Ng'ombe nisaidie!" Fisi alisema kwa huruma. Ng'ombe alimpa Fisi mkia wake mrefu ili ajishikilie atoke kwenye shimo hilo. Kwa furaha, Fisi alishika mkia wa Ng'ombe na kutoka ndani ya shimo.
Fisi alimshukuru Ng'ombe kwa usaidizi huo, kisha akamuomba ampe Ndama wake amle sababu alikuwa na njaa sana. Ng'ombe alishtuka na kumtupia Ndama wake macho.
Mwewe alipowaona wakibishana, alishuka chini na kuwauliza nini kilichotendeka. Ng'ombe alimjibu Mwewe na kumweleza kuwa alimsaidia Fisi kutoka ndani ya shimo ilhali alitaka kumla Ndama wake.
Mwewe alimwambia Fisi arudi ndani ya shimo amuonyeshe jinsi Ng'ombe alivyomsaidia.
Bila kusita Fisi aliingia ndani ya lile shimo tena. Ng'ombe na Ndama walimshukuru Mwewe kwa wema wake na kutorokea kichakani.

