

Hapo jadi jadudi palikuwa vijana wawili mapacha. Walihishi na mjomba wao. Siku mmoja waliamka asubuhi na kuchukua kifungua kinywa tayari kwenda shambani kupalilia mimea.
Mjomba wao aliwapakia chakula cha mchana kwenye kikapu.
Ghafla bin vuu, pakatokea nyani mnene mwenye meno ya kuogofya. Fira na kakake walipatwa na mshtuko na kuangusha kile kikapu.
Bila kusita, yule nyani alianza kula chakula walichokuwa wamebeba bila kubakisha chochote. Walikasirika na kuamua kukimbia nyumbani kumweleza mjomba wao kilichotendeka.
Baada ya kumweleza mjomba wao kilichotokea, alijawa na hamaki huku akikunja uso akiwaza jinsi ya kumfundisha nyani somo.
Fira na kakake waliamua kufuata ushauri wa mjomba wao. Kama ilivyokuwa desturi yao kwenda shambani, walibeba kikapu chenye uzito zaidi. Nyani aliwaona na kutoka mafichoni akiwa na furaha ribo ribo na kutabasamu jinsi kikapu kilivyojaa.
Bila kupoteza muda, nyani alinyoosha mikono yake ili aweze kukamata kikapu. Alipigwa na butwaa kuona kuwa vijana wale walimpa kikapu chao Kwa hiari.
Punde si punde, mbwa mkali aliruka kutoka kwenye kikapu na kumshambulia nyani bila huruma. Fira na kakake walifurahi kuona ushauri wa mjomba wao ulivyowasaidia. Tangu siku hiyo kuendelea, nyani alitoweka mahali pale na hakuonekana tena.
Fira na kakake walirudi nyumbani wakiwa na furaha tele tele kwa kuwa kile kizuizi kimeondolewa. Walimshukuru mjomba wao hivi wakigundua mjinga akierevuka, mwerevu yu mashakani.

