

Hapo zamani za kale paliishi Ng'ombe, ndama na Fisi.
Walikuwa marafiki wa kufa kuzikana.
Siku moja walipokuwa malishoni, Fisi alihisi kwamba haridhiki na chakula alichokuwa akila.
Alipokuwa anageuka ili amueleze Ng'ombe hisia zake, alianguka kwenye shimo lililokuwa karibu naye.
Kuona hivyo, Ng'ombe alidondokwa na machozi.
"Ng'ombe, nisaidie!" Fisi alisema kwa huruma. Ng'ombe alikimbia na kumpa Fisi mkia wake mrefu ili ajishikilie atoke kwenye shimo hilo.
Kwa furaha, Fisi alishika mkia wa Ng'ombe na kutoka ndani ya lile shimo.
Fisi alimshukuru Ng'ombe kwa usaidizi huo, kisha akamuomba ampe ndama wake amle sababu alikuwa na njaa sana.
Ng'ombe alishtuka na kumtupia ndama wake macho.
Mwewe alipowaona, alishuka chini na kuwauliza kwa nini walikuwa wamesimama hapo.
Ng'ombe akamjibu mwewe, "Nilimsaidia Fisi kutoka ndani ya shimo. Sasa anataka kumla ndama wangu."
Mwewe alimwambia Fisi arudi ndani ya shimo amuonyeshe jinsi Ng'ombe alivyomsaidia.
Bila kusita, Fisi aliingia ndani ya shimo tena.
Mwewe akawaeleza Ng'ombe na ndama
watorokee kichakani waokoe maisha yao.
Walimshukuru Mwewe kwa ushauri wake. Papo hapo walitorokea kichakani wakiwaza, "Kweli asante ya punda ni mateke."

