

Hapo zamani za kale, paliishi Mzee aliyeitwa Musa. Aliishi na familia yake. Musa alikuwa muwindaji hodari sana. Alitegemea kazi ya uwindaji kulisha familia yake.
Siku moja alienda msituni kutafutia familia yake chakula. Alitimua njia ya mkato kufika msituni.
Alipofika katikati ya msitu, alimwona Twiga kwa umbali. Alimnyemelea kimiakimia. Kumbe Twiga alikuwa amenaswa kwa mtego Musa aliokuwa ameuweka. Alijigamba moyoni akinena "siwezi kuja huku na nitoke bure".
Aliwaza na kiwazua jinsi atakavyomshika yule Twiga. Kwa kweli, alijua atarudi nyumbani na nyama ya kutosha kulisha familia yake pamoja na majirani.
Kimadaha, aliamua kumrushia mkuki alioubeba lakini kwa bahati mbaya mkuki ulikata kamba iliomfunga miguuni. Twiga ambaye sasa alikuwa katika hali ya kufa kupona hakusita. Aliruka na kuchana mbuga.
Musa alimrukia amshike. Twiga alimpiga mateke akaanguka chini pu! ungedhani ni mzigo. Ndipo akakumbuka, wahenga hawakutuchana nywele kwa mfupa wa samaki walipoketi kitako na kuloga kuwa mwenye nguvu mpishe.
Alijaribu kumshika mkia lakini wapi? Bidii yake iligonga mwanba. Twiga alitimua mbio huku akirukaruka. Kwake Musa, nyama ya Twiga iligeuka na kuwa ndoto ya mchana.
Alirudi nyumbani akiwa na mshangao na maswali chungu nzima familia yake itakula nini. Aliubeba mkuki wake huku akiwa na majeraha ya moyo, na kutembea mwendo wa kobe. Alihema kama mbwa aliyenusurika kumezwa na chatu.
Mzee Musa alikata tamaa na kuelewa kuwa kila mbwa ana siku yake.

