Hapo zamani palikuwa na Mzee Kobe. Aliishi peke yake kwenye nyumba ya matope. Siku Moja alihisi njaa sana na kwa vile alivyopenda maembe aliamua kwenda kuyatafuta. Jua nalo lilikuwa limewaka kweli kweli.
Alipokuwa njiani, aliona miti mitatu. Mti mmoja ulikuwa wa maembe mabivu. Alipoyaona akatabasamu. Papo hapo akaamua kuyaendea.
Alipanda juu ya mti akitarajia kuyachuma yale maembe ili ayale. Halikuwa jambo rahisi kwa Mzee Kobe kuukwea ule mti.
Baada ya kupanda juu, alijishikilia kwenye tawi la ule mti. Kobe huyu alikuwa na uzito kupita kiasi. Tawi halikustahimili uzito wake.
Tawi lile lilivunjika na Mzee Kobe akaanguka chini kwa mshindo pu! Ganda lake lililokuwa nyororo likapata nyufa.
Kobe alijutia kitendo chake cha kupanda mti. Alirudi nyumbani akiwa na njaa na hasira.