Mbuga ya Maasai Mara
Njeri Wachira

Tulianza safari yetu kutoka mji wa Nakuru. Tulipitia mji wa Naivasha na Mai Mahiu halafu tukaelekea Narok.

Barabara zote kutoka Nakuru hadi Narok zimewekwwa lami.

1

Kutoka Narok hadi Mbuga ya Maasai Mara ni kilomita themanini na nane. Barabara hii haina lami.

Ilituchukua masaa mawili kwa sababu ya ubovu wa barabara.

2

Ingawa ilituchukua muda mrefu kufika, nilifurahia safari kwani niliweza kuwaona wanyama wachache njiani.

Niliwaona mbuni, nyumbu, twiga, pundamilia, kondoo na ng'ombe wa jamii ya Wamaasai.

3

Tulipofika langoni, tulizingirwa na watu wengi waliokuwa wakiuza shanga na mapambo mengine.

Tulinunua shanga za aina tofauti: za kuvaa shingoni, masikioni na mikononi.

Pia, tulinunua viatu vya akala na shuka za kimasaai.

4

Tulipofika mahali tulikuwa tumepanga kulala, tulionyeshwa hema yetu.

Ilikuwa nzuri sana na yenye vitanda vilivyotandikwa shuka za kimaasai juu yake.

Pia, kulikuwa na neti ya kuzuia mbu.

5

Baada ya kuweka mizigo yetu, tulionyeshwa manyatta. Tuliingia ndani ya nyumba kadhaa na kuona jinsi Wamaasai wanavyoishi.

Nilishangaa kuona nyumba zao ndogo na tofauti sana na za kisasa.

6

Katika nyumba hizo ndogo, walikuwemo ndama pia.

Sikuona vitanda vya kisasa ila ngozi ya ng'ombe na moto wa kufukuza baridi usiku.

7

Walituimbia nyimbo zao za kitamaduni wakiwa wamevalia mavazi yao ya rangi nyekundu na shanga maridadi.

Pia, walitufunza jinsi ya kuwasha moto bila kiberiti. Walisugua vijiti viwili pamoja mpaka moshi ukatoka.

8

Tulirejea kwenye makazi yetu na kupata tumeandaliwa mlo.

Baada ya kula, tulielekea kwenye hema zetu na kulala.

9

Usiku wa manane tuligutushwa na mlio mkali wa kutisha. Baba alinieleza kuwa ulikuwa wa simba.

Nilishikwa na wasiwasi na kumshika baba mkono. Alinifariji kwa kunieleza kuwa kuna walinda zamu ambao wangewafukuza simba.

10

Baadaye, tulisikia fisi akilia kutoka mbali lakini kilio chake hakikutisha kama kile cha simba.

Nilishikwa na usingizi nikalala mpaka kulipopambazuka.

11

Asubuhi, tuliingia katika gari la mbugani na kuelekea kwenye nyika kutafuta wanyama.

Tulifika pahali mto wa Mara ulipoonekana.

12

Tuliwaona viboko katika mto wa Mara. Tulihesabu: mmoja, wawili, watatu…hadi thelathini.

Walikuwa wametulia tuli wakiota jua.

13

Baadaye, tuliarifiwa na madereva wengine kuwa simba walikuwa wameonekana. Tulitimua kuelekea tulikoelekezwa.

Tuliwapata simba watano wakimrarua pundamilia.

14

Nilihofu kwani gari letu lilikuwa paa wazi. Dereva alinituliza na kusema kuwa wasiposumbuliwa hawawezi kutudhuru.

Ni kweli! Waliposhiba, walilala kando ya nyama iliyobaki. Hawakujali magari yaliyokuwa yamewazunguka.

15

Tuliendelea na safari yetu ya kuwatafuta wanyama.

Tulikutana na kundi la tembo waliokuwa wamepiga mstari wakivuka barabara.

Dereva aliendesha kasi ili tukaribie tuwaone tembo vizuri.

16

Tulishangaa tulipomwona tembo aliyekuwa mnene kuliko wote, akigeuka na kuanza kuja upande wetu mbio.

Dereva alirudi nyuma upesi kama risasi. Nilipiga mayowe nikifikiri tungeangamia.

17

Baada ya dakika chache, tembo aligeuka na kwenda kuwatafuta wenzake.

Kumbe, tulimkasirisha kwa kelele za gari akafikiria sisi ni adui!

18

Ghafla bila kutarajia, tulikutana na simba wawili.

Dereva alituambia ni harusi. Alikuwa simba wa kiume na wa kike.

19

Tulirejea makazi yetu kama tumechoka kabisa.

20

Tulishika barabara na kurudi mjini Narok halafu tukachukua njia kuelekea Kisii.

21
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Mbuga ya Maasai Mara
Author - Njeri Wachira
Illustration -
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs