

Tulitamani sana kuliona ziwa la Bogoria kwa sababu tulikuwa tumesikia sifa zake kutoka kwa watu wengi. Tulichukua gari kutoka Nairobi na kusafiri kilomita mia tatu.
Njiani tuliweza kuona wanyama tofauti kama vile nyoka na kobe kando kando mwa barabara.
Tuliona miti ya aina ya mishita kando kando mwa barabara. Mishita ina miiba mingi sana. Pia tuliona miamba mikubwa njiani.
Tulipofika kwenye ziwa tulilipa ada langoni na kuingia.
Nilishangaa sana kuona aina nyingine ya miti iliyokuwa na matunda mekundu. Nilielezwa huitwai miti ya pilipili.
Tuliona nyumba kubwa ya mchwa iliyoundwa kwa mchanga karibu na lango.
Ndani ya mbuga tuliona nyumba zingine nyingi za mchwa.
Ndani ya mbuga tulienda kwenye ziwa kuwaona heroe ambao walirembesha ziwa kwa rangi yao ya maridadi ya waridi.
Halafu tulienda kwenye chemichemi zenye maji moto. Nilipoambiwa kuwa maji yaliyokuwa yakiruka yalikuwa moto sikuamini. Nilidhani ni utani tu.
Mjomba alitoa mayai ya kuku na kuyaweka ndani ya maji yaliyokuwa karibu na chemichemi. Alingoja kama dakika ishirini kisha akanipa yai moja nile.
Nilitoa maganda yake nikijihadhari ili nisimwagikiwe na yai. Lakini lo!
Nilipata kuwa yai lilikuwa limeiva.
Nikala huku nikitabasamu kwa mshangao.
Mwishowe tuliangalia waimbaji wa kabila
la kitugeni wakiimba nyimbo zao za kitamaduni.
Walitukaribisha kujiunga nao na tukashika mikuki, ngao na pembe.
Jioni ilipofika tulirudi nyumbani.

