

Hii ni Shule ya Nakivale. Ilitokea kwamba mwanafunzi mmoja aliyeitwa Nkanu, aliambukizwa ugonjwa wa kipindupindu. Ilisemekana kwamba maambukizi hayo yalisababishwa na uchafu.
Wakati wa kwenda nyumbani ulipofika, wanafunzi walianza kwenda. Nkanu aliruka kwa furaha kwa sababu wakati alioupenda ulikuwa umefika.
Nkanu alikuwa ameweka vitu vyake kwenye begi ndogo aliyoibeba kila siku.
Alipofika nyumbani, Nkanu hakutulia hata kidogo. Alikwenda kuchezea udongo mchafu.
Baadaye, mvua ilianza kunyesha. Nkanu hakujikinga na mvua hiyo. Aliendelea kucheza bila kujali kwamba alikuwa akilowa.
Nkanu alipofika nyumbani, hakunawa mikono yake. Wakati wa kula ulipofika, alienda kula hivyo hivyo kwa mikono michafu.
Nkanu alipomaliza kula, alienda barabarani kutembea. Alimwona mtu aliyekuwa na ndizi. Nkanu alimwomba yule mtu ndizi. Alipoipokea ile ndizi, aliila hivyo hivyo kwa mikono michafu.
Hiyo ndiyo iliyokuwa tabia ya Nkanu ya kila siku. Baada ya siku chache, Nkanu alianza kuhisi maumivu. Kumbe alikuwa ameambukizwa kipindupindu.
Nkanu alitapika na kuendesha. Alitamani achezee tope tena lakini hakuwa hata na nguvu ya kuweza kusimama. Alikuwa mnyonge kweli kweli.
Nkanu alikumbuka makosa aliyoyafanya. Alitaka kujua ni lini hasa alipoambukizwa viini vya kipindupindu. Alisema moyoni, "Heri ningejua, ningenawa mikono yangu kabla ya kula."

